Hamas walikuwa na mpango uliopangwa wa kutumia unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita, mwanaharakati wa haki za wanawake wa Israel na mwanasheria amesema.
Prof Ruth Halperin-Kaddari alisema aliona picha za wanawake katika maeneo kadhaa ambao hali zao zilionesha "bila shaka" kwamba walibakwa.
Kumekuwa na hasira juu ya kuchelewa kwa baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kukiri madai ya unyanyasaji wa kijinsia wa Hamas tarehe 7 Oktoba.
Israel imekuwa ikichunguza ushahidi wa uhalifu wa kingono wakati wa mashambulizi hayo.
Polisi wa Israel wanasema hadi sasa wamekusanya ushahidi zaidi ya 1,500 kutoka kwa mashahidi na matabibu.
Hamas imekanusha kundi hilo kutekeleza unyanyasaji wa kingono wakati wa mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.
Picha na video za moja kwa moja zilizotiririshwa na wanamgambo hao ziliashiria hali ya kutisha ya mashambulizi katika tamasha la Supernova. Vurugu mbalimbali kuanzia ubakaji wa magenge hadi ukeketaji wa waathiriwa waliouawa zinachunguzwa na polisi.
"Niliona mashuhuda kadhaa, kwa mfano wa mtu mmoja aliyenusurika ambaye alijificha vichakani na kumwona mwanamke karibu naye akibakwa na wanaume kadhaa," Prof Halperin-Kaddari aliambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4.
Alisema pia alizungumza na mhudumu wa afya ambaye alimtibu mwanamke aliyepoteza kiasi cha damu kilichotishia maisha yake baada ya kuripoti kubakwa na wanaume wanne.
"Niliona picha kutoka sehemu nyingi za miili ambayo hali zote zilikuwa zikionesha mtindo sawa wa ukeketaji na bila kuacha shaka kuwa ubakaji ulifanywa kwa wanawake hao kabla ya kunyongwa," alisema.
Prof Halperin-Kaddari aliongeza kuwa wingi wa kesi, zote kwa siku moja lakini katika maeneo kadhaa ulimwacha "bila shaka" kwamba kulikuwa na "matayarisho ya kutumia unyanyasaji wa kingono kama silaha ya vita."
0 Comments