Waisraeli watatu waliuawa na 16 kujeruhiwa baada ya watu wawili, Wapalestina kufyatua risasi kwenye kituo cha mabasi kilichojaa watu huko Jerusalem Magharibi, polisi wa Israel wamesema.
Video ya CCTV ilionesha washambuliaji hao wakishuka kwenye gari kwenye barabara kuu na kuwapiga risasi watu waliokuwa wamesimama kwenye lami wakiwa na bunduki na bastola.
Askari wasiokuwa zamu na raia katika eneo la tukio waliwaua watu wenye silaha, ambao polisi walisema walikuwa wanatoka Jerusalem Mashariki inayokaliwa.
Waziri wa usalama wa taifa wa Israel alisema walikuwa "washirika wa Hamas". Hakukuwa na taarifa ya mara moja kutoka kwa Hamas, ambayo saa chache kabla ya hapo ilikuwa imekubaliana na Israel kuongeza muda wa mapatano katika Ukanda wa Gaza kwa siku ya saba na kuruhusu kubadilishana tena mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken wakati huo huo aliwasili Tel Aviv kama sehemu ya juhudi za kuongeza muda wa kusitisha vita hivyo vikali, vilivyochochewa na shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.
Siku ya Alhamisi asubuhi Bw.Blinken alifanya mazungumzo na Rais wa Israel Isaac Herzog, ambaye alimweleza kuwa ufyatulianaji risasi wa Jerusalem ni mfano mwingine wa "vita visivyoisha ambavyo tunapigana dhidi ya mashirika ya kigaidi, hasa Hamas, katika nyakati hizi ngumu na zenye changamoto".
Bw Blinken alisema shambulio hilo lilikuwa ukumbusho "wa tishio la ugaidi ambalo Israel hukabiliana nalo kila siku".
