Bilioni 278.8 kumalizia miradi ya maendeleo Manyara.



Na John Walter- Manyara 
Mkoa wa Manyara umepokea jumla ya shilingi bilioni 278.8 kutoka serikali kuu, fedha ambazo zinajumuisha matumizi ya kawaida na matumizi kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka 2024.

Hayo yameelezwa leo machi 15,2024  na
Kaimu katibu tawala msaidizi mipango na uratibu ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara Lusungu Mwilongo katika kikao cha 37 cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Manyara.

Kikao hicho chenye lengo la kupitia na kukagua ripoti ya maazimio ya kikao kilichopita na kujadili mipango ya miradi ya maendeleo ya taasisi za Umma ndani ya mkoa wa Manyara pamoja na bajeti ya mkoa, amesema vipaumbele ni kukamilisha miradi viporo, kudumisha amani na usalama, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kujiandaa na chaguzi za serikali za mitaa zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.



Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amewataka wakuu wa taasisi, wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Amesema utekelezaji wa miradi kwa wakati utaleta nafuu kwa wananchi kwani itasaidia kutatua kero zao, hivyo kuchelewa kwa miradi kutaendelea kudidimiza ustawi wa wananchi wa mkoa wa Manyara.

Aidha amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Manyara kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zote zinawekwa benki kwa wakati na kuacja mara moja tabia ya fedha za serikali kukaa mikononi mwa mtu kwa muda mrefu.

'Kwa mujibu wa taratibu za ukusanyaji wa mapato, fedha haipaswi kukaa mikononi mwa mwa mtu zaidi ya saa 24 lakini Kuna baadhi ya halmashauri Hela hazijawekwa kwenye akaunti tangu mwaka Jana, hii sio sawa naomba mjirekebishe na muwasimamie vizuri watendaji wenu' alisisitiza Sendiga

Post a Comment

0 Comments