DARAJA LA MINYUGHE, WILAYANI IKUNGI, SINGIDA KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI


Ikungi

Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha Kata ya Minyughe na Makilawa, katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida, lililokatika miaka mitatu iliyopita, na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu. 

Kukamilika kwa daraja hilo la chuma (Mibey Bridge) lenye urefu wa mita 30 lililogharimu zaidi ya Sh. Bilioni 1.6/-katika barabara ya Mtamaa-Minyughe hadi Mtavira, Wilayani Ikungi, litaenda kufungua fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa kata hızo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahim Kibasa, alisema kukamilisha uunganishaji wa vyuma kwa ajili ya daraja hilo, kumewezesha mto Minyughe kufunguka, na hivyo kutoa fursa kwa shughuli za uchukuzi kuendelea kati ya maeneo ya vijijini na makao makuu ya mkoa.

Mhandisi Kibasa alisema kuwa, sasa wananchi wa kata tatu zinazounganishwa na daraja hilo, wataweza kuzikabili changamoto mbalimbali, zilizokwamisha shughuli zao, hususani wakati wa masika, kutokana na mto kufurika maji, kiasi cha kutishia usalama wao wakati wa kuvuka.

" Sehemu ya fedha hizo ni bajeti mwaka ya mwaka huu ambapo tumejenga  madaraja ikiwemo  daraja hili la Minyughe,daraja hili limekuwa likiwasumbua wananchi takribani miaka mitatu na hivyo kukwamisha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kata tatu pamoja na Mkoa wa jirani wa Tabora, katika wilaya ya Uyui, inayopakana na wilaya hii ya Ikungi, "alisema.
** 
Aidha, Mhandisi Kibasa alisema, ujenzi wa daraja hilo umetokana na bajeti ya mwaka iliyotengwa, kiasi cha Sh. Bilioni 4.4/- katika wilaya ya Ikungi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja, katika halmashauri ya Wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia kukamilika kwa kazi hiyo, akiwemo Bi. Elizabeth Bakari wa Kijiji cha Minyughe, na diwani wa Kata Minyughe , Mhe. Nelson Kiwesi, waliishukuru Serikali kwa mradi huo, ambao baada ya kukamilika, unakwenda kuondoa adha ya usafiri, hasa kwa wajawazito.

Bi. Elizabeth alibainisha kuwa, iliwalazimu kukosa huduma muhimu ikiwemo zile za afya katika kituo cha afya kilichopo ng'ambo ya pili, pia watoto wao kuhatarisha maisha wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani, hususani nyakati za masika, kutokana na mto Minyughe kufurika maji.

Alisema kukamilika kwa daraja hilo, sasa watoto wao hawatakosa masomo, wajawazito na wagonjwa wataenda kupata Huduma za matibabu kwenye kituo cha afya kilichopo ng’ambo ya daraja hilo pamoja na kufungua shughuli za usafirishaji wa mazao na watu.

“Kujengwa kwa daraja hili, ni mafanikio makubwa kwa watoto wetu waliolazimika kushindwa kuhudhuria vipindi vya masomo yao darasani. Serikali itaongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi , ikiwemo kilimo, na mali asili kupitia misitu, wazalishaji wamerahisishiwa mawasiliano kati ya upande mmoja na ule wa pili," alisema.

Awali Mhandisi Mshauri Ebenezer Mollel, kutoka TARURA makao makuu, kitengo cha madaraja, alisema daraja hilo ni la tatu kujengwa hapa nchini, likitanguliwa na mengine lililopo Kihansi, huko Kilombero na lile la Mbuchi, kule Kibiti, mkoani Pwani.

Mhandisi Mollel alisema kuwa, madaraja hayo ni ya aina ya kipekee, hivyo kabla ya ujenzi hulazimika kuwapatia mafunzo Wahandisi wa TARURA na TANROADS, lengo likiwa kuwajengea uwezo, kwa ajili ya kupata ujuzi na utaalamu zaidi kuweza kumudu majukumu yao, kulingana na kukua kwa teknolojia, huku wahandisi walioshiriki mafunzo hayo, wakifikia 42.

Kwa mujibu wa mhandisi Mollel, teknolojia ya daraja hilo ni ya kipekee, kutokana kujengwa likiwa ng'ambo ya pili, na baada ya kukamilika husukumwa hadi sehemu yake, kuunganisha kingo mbili, na kuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya kivuko.

Post a Comment

0 Comments