Mkuu wa wilaya ya Njombe akutana na CHADEMA ofisini kwake na kuwasikiliza kisa risiti feki






News
Njombe

Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Njombe kubaini uwepo wa risiti feki walizopewa wananchi wa kata ya Iwungilo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya na michango mingine,Mkuu wa wilaya ya Njombe amelazimika kuwaita viongozi wa Chama hicho na kusikiliza changamoto hiyo.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa CHADEMA Chini ya mwenyekiti wao wa mkoa Rose Mayemba  na baadhi ya wananchi wa Iwungilo kimebainisha namna ya kuchukua hatua dhidi ya Malalamiko ya wananchi hao.

Awali viongozi wa Chadema Rose Mayemba na Regnard Danda wamesema katika kata ya Iwungilo mbali na changamoto ya Risiti feki lakini kuna malalamiko mengi ya Wananchi dhidi ya Viongozi wa Vijiji na Kata ambayo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.

"Wananchi wamechimba mchanga lakini ripoti hii haionyeshi kama ni fedha za wananchi ila mwenyekiti wa kijiji ndio aliyekuwa mzabuni akalipwa ile fedha nguvu ya wananchi na sio tu nguvu ya wananchi sasa hizi risiti feki fedha zake humu kwenye ripoti hazipo"amesema Rose Mayemba Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe

Baadhi ya wananchi wa Iwungilo wakiwemo waliolipishwa michango na kupewa risiti feki akiwemo Gustaf Mtewele Betina Mgina na Melsiana Mtewele wamesema vitendo wanavyofanyiwa huko kijijini vinawakwaza pakubwa na kuiomba serikali kuingilia kati.

Akizungumza kwa Niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe bwana Izack Mapunda amekiri kuwa risiti hizo sio za halmashauri ya mji na kwamba wataenda kufanya ukaguzi kuona matumizi ya fedha hizo.

"Inatakiwa zitoke risiti za halmashauri lakini changamoto tunayokutana nayo anayeprint zile risiti za halmashauri ni mtu mmoja tu kwa kuna wakati risiti zainachelewa kutokana na mazingira kwa hiyo serikali ya kijiji lazima iwe taarifa hiyo na lazima wawaambie wananchi"amesema Mapaunda

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amekiri kuziona risiti  hizo bandia na kwamba atakwenda kufuatilia kuona uhalisia wake na kuchukua hatua.

"Kwa hiyo hivi vitu ambavyommevieleza tunavichukua na kwenda kuvifanyia kazi na nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananjombe wote wenye kero kwamba ofisi iko wazi na sisi tupo hapa kwa ajili ya kuwatumikia"amesema DC Kissa

Post a Comment

0 Comments