Mradi wa uanagenzi Pacha na Mitambo wakamilika kwa Mafanikio Makubwa.


Na John Walter-Manyara

Vijana wameaswa kutumia vyema mafunzo ya uanagenzi pacha katika fani ya mitambo na zana za kilimo waliyopata katika vyuo vya VETA kupitia mradi uliofadhiliwa na shirika la Ujerumani la WHKT ili waweze kujiajiri na kuonesha bayana walichojifunza katika kipindi chote.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa mafunzo ya ufundi stadi VETA Abdallah Shaban wakati akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa VETA katika hafla ya ufungaji wa mradi wa mafunzo ya uanagenzi katika fani ya mitambo na zana za kilimo iliyofanyika katika chuo cha VETA Manyara, ambapo amesema  imekuwa fursa kubwa  kwa vijana na itasaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kufanya kilimo bora na chenye tija kutokana na utaalamu waliojifunza ikiwemo kutumia vizuri mitambo ya kisasa ya kilimo.

"Tunataka kuona vijana wanajiajiri na kupata kazi kutokana na mafunzo haya yaliyotolewa na hata kwa walimu, pia tunategemea walichojifunza kionekane dgahiri kupitia shughuli zao za kilimo" alisema Abdallah

Kwa upande wake Mhandisi Ezekieli Kunyaranyara kutoka wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi amepongeza maendeleo ya mradi kwani ni sehemu ya kutekeleza sera ya elimu nchini kwa kuwaongezea watanzania ujuzi kwenye fani mbalimbali ikiwemo kilimo licha ya idadi ya uwepo wa idadi ndogo kwa wanawake.

Kunyaranyara ameongeza kuwa kukosekana kwa idadi kubwa ya wanawake katika fani za kilimo kumeifanya serikali kuja na mtazamo mpya wa kuwapa kipaumbele  katika udahili  kuanzia asilimia hamsini hadi sitini na hii itaelekezwa kwa vyuo vya VETA ili waanze kuzingatia utaratibu huo.

Aidha amesema serikali inaendelea kujenga vyuo vipya vya mafunzo ya ufundi stadi na hivi sasa kuna vyuo 80 huku vyuo vingine 65 vikitarajiwa kujengwa mwakani na kufanya kuwa na jumla ya vyuo 145 vya ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanaendelea kupata fursa za mafunzo nchini.

Mwanzilishi wa mradi kutoka nchini Ujerumani Herman Roder amesema mradi huo umefanikisha kutoa matokeo chanya yaliyotarajiwa na kwamba ameridhishwa na utekelezaji wa mradi katika kipindi cha miaka sita katika chuo cha VETA Manyara na maeneo mengine yanayotekeleza mradi.


Jitu Vrajlal Son ni makamu mwenyekiti wa baraza la kilimo taifa ambae pia ni mnufaika wa mradi huu kwani yeye ni mkulima na ameajiri vijana kwenye vitengo tofautitofauti ikiwemo kwenye karakana ya zana za kilimo, kuongoza mitambo na  uchomeleaji na kwa upande wake amekiri ubora wa wanafunzi waliopata mafunzo hayo kwani wanauwezo mkubwa wa kufanya kwa vitendo kile walichojifunza ambapo kwa sasa ndio hitaji kubwa la soko.

Jitu amesema kuwa na ujuzi  ni kitu muhimu zaidi kuliko kuwa na vyeti ambavyo hauwezi kuvifanyia kazi, hivyo ameiomba serikali kutoa mikopo ya mitaji kwa wanafunzi wa VETA kutoka kwenye kodi ya mafunzo ya ujuzi inayolipwa na sekta binafsi maarufu SDL ili waweze kujiajiri wenyewe kuliko kutoa mikopo kwa vyuo vya elimu ya juu pekee kwani nguvu kazi inayohitajika ipo kwenye mafunzo ya ufundi stadi.

Mradi wa mafunzo ya uanagenzi pacha katika fani ya mitambo na zana za kilimo ni mradi uliodumu kwa takribani miaka sita tangu ulipoanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2023 ukijumuisha vyuo vitano vya VETA nchini kwa kushirikiana na  shirika la kijerumani la WHKT.

Kwa hivi sasa mradi huo umetamatika lakini utoaji wa mafunzo utaendelea chini ya vyuo vya VETA baada ya kuamua kuundeleza mafunzo hayo kupitia walimu waliopata fursa ya kwenda nchini Ujerumani kujifunza na sasa ni jukumu lao kuhamishia maarifa hayo kwa wanafunzi. 


Post a Comment

0 Comments