Mrembo Sara anyakua taji la Miss Sed 2024,apewa gari


Na John Walter -Manyara

Sarah David wa (19) ameshinda taji  la shindano la urembo  ‘Miss Sed 2024’ na kuwaongoza warembo wenzake 15 waliowania taji hilo.

Kufuatia ushindi huo amekabidhiwa zawadi ya gari aina mpya ya VITZ na shilingi Milioni moja na ajira katika Kampuni ya Mati super Brands Ltd kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Sarah David amepokea taji hilo kutoka kwa Jennifer Mmari wa Arusha aliyekuwa akilishikilia.

Mshindi wa pili ni Gisela Charles ambaye amepatiwa shilingi Milioni mbili huku mshindi wa tatu Sabrina Mselemo akipewa shilingi Milioni moja.

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amempongeza mdhamini wa mashindano hayo David Mulokozi kwa kuamua kuinua vipaji vya vijana kwa kuwapa motisha kwa kile wanachokifanya.

Twange amesema Kampuni hiyo imekuwa msaada kwa vijana na serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa kila jambo.

Naye mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited  David Mulokozi ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo amesema kuwa kampuni hiyo imejifungamanisha na jamii na kuunga mkono masuala mbali mbali ya kijamii ikiwemo mashindano hayo ya Miss Sed 2024  ambayo  yanalenga kutoa fursa kwa vijana wa kike.

Mwandaaji wa mashindano hayo Hamis Masongo (Shaba Entertainment) amesema urembo ni ajira hivyo wazazi wawaruhusu mabinti zao kushiriki kwenye mashindano hayo yanapotangazwa.

Shindano hilo kubwa la urembo mkoani Manyara kwa mwaka huu limefanyika katika ukumbi wa Chuo kikuu huria Manyara uliopo miomboni kata ya Bagara mjini Babati.

Post a Comment

0 Comments