Mwanafunzi wa darasa la pili ajinyonga Babati.



Na John Walter-Babati
Katika hali isiyo ya kawaida mtoto wa umri wa miaka nane mkazi wa mtaa wa Mruki katika mji wa Babati mkoani Manyara, amejinyonga kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuchukizwa na ugomvi kati ya baba na mama.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa mtaa wa huo Abdilahi Rajabu, tukio hilo limetokea majira ya saa saba mchana Machi 16,2024 ikiwa ni siku ya nne tangu mama mzazi wa marehemu aondoke nyumbani kutokana na ugomvi wa kila mara kati ya baba na mama. 

Mtoto huyo amejinyonga kwa mkanda katika mti wa mstafeli uliopo nje ya nyumba yao.

Amesema baba wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Adamu Abdallah amekuwa na ugomvi na mkewe mara kwa mara kutokana na wivu wa mapenzi (kutoaminiana) na kwamba wamekuwa wakigombana mbele za watoto hata mara ya mwisho Adamu alimnyang'anya mkewe ufunguo wa nyumba mbele za watoto. 

Akizungumza na Muungwana Blog, Baba wa mtoto huyo amekiri kuwepo ugomvi kati yake na mkewe na kwamba ni kweli watoto walikuwa wanafahamu tofauti kati yake na mkewe lakini hakutarajia kufikia hatua hiyo. 


Mwili wa Mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la pili katika shule ya msingi Maisaka  mjini Babati umechukuliwa na polisi kwa ajili ya kuhifadhiwa wakati uchunguzi ukiendelea. 

Post a Comment

0 Comments