Waziri Masauni aipongeza Orxy Gas kwa kugawa mitungi 700 bure kwa baba na Mama Lishe

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (wa pili kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (wa kwanza kushoto) wakimkabidhi mtungi wa kupikia wa gesi ya Orxy Adhuruu Makame Kombo katika hafla ya ugawaji wa mitungi 700 ya kupikia ya Oryx kwa baba lishe na mama lishe Machi 13, 2024 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Visiwani Zanzibar.

WAKATI Serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Yusuf Masauni kwa kushirikiana na Kampuni ya gesi ya Oryx wamegawa mitungi 700 ya gesi kwa wananchi wakiwemo Baba na Mama Lishe visiwani Zanzibar.

Akizungumza leo Machi 13,2024 wakati wa kugawa mitungi hiyo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar, Waziri Masauni amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuchukua hatua  mbalimbali.

Hivyo amesema kitendo cha Oryx kushirikiana naye kugawa mitungi hiyo bure kwa wananchi wa Jimbo la Kikwajuni kunakwenda kusaidia kuifanya jamii hiyo kuachana na kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi ambayo inafaida nyingi.

“Tunaamini waliopata majiko haya gesi pamoja na kupatiwa mafunzo ya namna ya kuyatumia watakuwa mabalozi wazuri kwa kuwahamasisha wananchi wengi zaidi wa Zanzibar na Tanzania wahame sasa kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa na waje katika kutumia gesi.

“Faida ya kutumia gesi ni nyingi tumezoa kutumia mkaa tukiamini tukaokoa fedha lakini kimsingi kwa mujibu wa maelezo ya watalaam gharama za matumizi ya mkaa ni kubwa zaidi ukilinganisha na gesi.

“Hakuna sababu ya mtu kutumia kuni au mkaa ambao unakwenda kuleta madhara ya kiafya na mazingira,”amesema Waziri Masuni na kusisitiza umefika wakati kwa jamii kubadilisha fikra kwa kujikita katika kutumia nishati safi ya kupikia.

Ameongeza waliopata mitungi hiyo kwa awamu ya kwanza ni wananchi 700 na matamanio yake ni kuona wananchi 24000 wa jimbo la Kikwajuni wanapata nishati safi ya kupikia hasa gesi.

Amesisitiza  wananchi wa jimbo la Kikwajuni wako  mjini hivyo lazima waende na kasi ya mabadiliko ya mtazamo wa Serikali wa kuhamasisha nishati safi ambayo ni rafiki zaidi ili kuepuka nishati chafu zinazosababisha madhara.

Awali Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema wanaamini ukipika kwa kutumia gesi, inaleta maendeleo mengi kwa jamii yetu sambamba na kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti.

“Zaidi ya yote ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa.Hivyo tunakushuru Waziri Masauni kwa kushirikiana nasi katika kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Kikwajuni wanapata niashati safi ya kupikia.”

Pia kutumia gesi ya Oryx kunawezesha  watoto kuwa na muda mwingi zaidi kusoma na sio kwenda kutafuta kuni huku akisisitiza kutumia gesi kunaepusha wamama na watoto kuumia kwa kubeba kuni nzito na kuepuka kujeuriwa na Wanyama wakali wakiwa wanatafuta kuni.

Aidha amesema kwa miaka mingi Oryx Gas imekuwa kampuni kiongozi katika kukuza matumizi ya gesi nchini Tanzania na kuanzia mwaka Julai mwaka 2021 wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali.

Amefafanua maelekezo hayo yaliyopokea kutoka kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Kupitia mipango hii, Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo si tu mbaya kwa afya zetu bali pia ni hatari kwa mazingira yetu na Oryx inatekeleza juhudi za kueneza matumizi ya nishati safi kwa Watanzania wengi ipasavyo ambayo ni ndoto kubwa ya Rais Mama Samia.

Ameongeza Oryx Gas Tanzania inajipongeza kwa kujulikana kuwa kampuni kinara katika usambazaji wa gesi ya kupikia kwa Watanzania kwa sasa na kwamba wataendelea kuwekeza zaidi katika kuratibu kubadilisha na kueneza nishati safi kutumika kwa wananchi wengi.

Araman amesema Oryx Gas inajulikana kwa kuuza mitungi ya gesi pamoja na kufunga mifumo salama ya gesi kwenye taasisi na viwanda vinavyotumia gesi kwa wingi.

“Hivi majuzi tumezindua mfumo wa gesi katika shule ya Sekondari ya Hasnuu iliyopo Kizimkazi. Kupitia mipango ya kusambaza nishati safi ya kupikia, Oryx Gas itaendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi katika familia, taasisi zenye watu zaidi ya 100 na viwanda.

Aidha amesema anamshukuru Waziri Masauni kwa kuwa balozi mzuri wa kuleta maendeleo kwa jamii kiujumla kwa kuwaunga mkono katika mpango huo wa matumizi ya nishati safi katika jimbo la Kikwajuni.

Wakati huo huo Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Gas Peter Ndomba pamoja timu nzima ya kampuni hiyo wametoa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia lengo likiwa kuiwezesha jamii kuwa salama na kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa kutokuwa na uelewa wa kutumia mtungi wa oryx.

Akizungumza mbele ya wananchi waliopatiwa mitungi na majiko yake, Ndomba amesema pamoja na kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi matumizi sahihi ya gesi ni kipaumbele chao na wamekuwa wakitoa mafunzo kabla ya kugawa mitungi.

Post a Comment

0 Comments