DC Babati: Viongozi watumikieni wananchi bila kuwabagua.


Na John Walter-Babati

WANANCHI wa kijiji cha Haysam wilaya ya Babati mkoani Manyara wameeleza kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa kijiji hicho Martin Safari Deemay kutokana na matumizi mabaya ya madaraka ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu wa mali za kijiji.

Wameeleza kuwa ubadhirifu huo aliufanya akiwa madarakani tangu mwaka 2021 mpaka sasa huku wajumbe na wananchi wakikosa haki ya kuhoji.

Hayo yamebainika katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Dareda.

Hoja zinazowafanya wananchi hao kutokuwa na imani na Mwenyekiti wao ni pamoja na  kushindwa kusimamia mali za kijiji, kushindwa kuonyesha ushirikiano na wajumbe wa halmashauri ya kijiji, kuwa chanzo cha migogoro badala ya kuwa mtatuzi na kushindwa kusimamia usomaji wa mapato na matumizi ya kijiji kwa mujibu wa sheria.


Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewataka viongozi waliochaguliwa na wananchi kuwatumikia wananchi wote bila kubagua tofauti zao ili kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.

Twange amemweleza mwenyekiti huyo mbele ya wananchi, kwa siku zilizobaki ajitathimini kama kweli anatosha kuwa kiongozi wa  kijiji hicho.

Aidha aliongeza kuwa, suala la kumuondoa Mwenyekiti madarakani pamoja na wajumbe wa Serikali, kwa  mujibu wa taratibu na kanuni zilizotungwa mwaka 1995, wenye mamlaka ya kumuondoa Mwenyekiti ni Halmashauri ya Serikali ya Kijiji yenye watu 25 kwa kupiga kura mara baada kupitia tuhuma zilizopatikana kwenye mikutano mikuu ya Vijiji kwa wananchi ambao walimchagua.

"Tatizo ni kwamba hata nusu ya wajumbe haijafika, tuingweza kufanya maamuzi leo, siku mkikamilika mniite tumuondoe huyo mwenyekiti msiomtaka, ila kwa sasa vikao viendelee kufanyika kwa kumteua mwenyekiti wa muda atakaeongoza vikao ili shughuli zenu za maendeleo zisikwame" alisisitiza mkuu wa wilaya Lazaro Twange

Mkuu wa wilaya Lazaro Twange anaendelea na ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kata kwa kata akiongozana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, Jeshi la Polisi, idara ya maendeleo ya jamii, Ustawi wa jamii, Maafisa Elimu,TANESCO, TARURA,RUWASA ili kujibu hoja za wananchi.

Halmashauri ya wilaya ya Babati ina kata 25 huku ya mji ikiwa na kata 8.

Mwenyekiti anayetuhumiwa akijibu hoja za wananchi katika mkutano huo.


Post a Comment

0 Comments