HakiElimu yatoa mapendekezo kwa Serikali upangaji, utengaji bajeti sekta ya elimu 2024/25


Taasisi ya HakiElimu imetoa mapendekezo kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu kutenga Bajeti mahususi kwaajili ya kuhuisha mpango wa tatu wa Maendeleo ya Sekta ya elimu na kuandaa mpango wa nne wa Maendeleo ya Sekta ya elimu katika mwaka wa fedha kwenye sera na Mtaala husika.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dkt. John wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2024 Jijini Dar es Salaam, amesema Serikali inapoelekea katika upangaji wa Bajeti ya Sekta ya elimu kwa mwaka mpya wa fedha 2024/25 inapaswa kuzingatia mchakato wa utengenezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa 2025 lakini pia kuanza kwa utekelezaji wa mitaala na sera mpya ya elimu 2023.

"Kama serikali inakusudia kuanza utoaji wa Tahasusi hizo zote ni muhimu kupanga na kutenga Bajeti maalum katika mwaka wa fedha 2024/25 kwaajili ya mambo mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo kazini kwa walimu waliopo, kuajiri walimu wapya wenye ujuzi na umahiri katika Tahasusi husika lakini pia kuwa na mpango maalumu wa Kuhamasisha udahili wa wanafunzi wa ualimu vyuoni ili kuendelea kutengeneza walimu wenye ujuzi kulingana na mabadiliko hayo". Amesema 

Ameongeza kuwa serikali pia itenga Bajeti  kwa ajili ya kutoa mafunzo kazini kwa walimu waliopo ili waweze kusaidia utekelezaji wa tahasusi na kuajiri walimu wapya wenye ujuzi umahairi katika tahasusi husika ikumbukwe kuwa hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika shule  za sekondari yalikuwa ni 174,632 ambapo walimu waliopo ni 84,700 na upungufu wa walimu 89,932 sawa na asilimka 51.5%".

Aidha HakiElimu pia imependekeza Bajeti kwaajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu vya Kiada shuleni, ambapo wameiomba serikali katika Bajeti ya Sekta ya elimu mwaka wa fedha 2024/25 watenge Bajeti maalumu kwaajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu hivyo mashuleni hasa kwa kuzingatia kuwa vitabu hivyo ni vipya hivyo shule hazina akiba ya vitabu mbadala.

Pia wameiomba serikali kuweka mpango maalumu wa usambazaji wa vitabu hivyo mashuleni ukiainisha muda mahususi wa ukamilishaji wa zoezi hilo

Mbali na hayo, Hakielimu wamependekeza ujumuishi wa teknolojia katika utekelezaji wa mtaala mpya wa Elimu, ambapo imeishauri serikali kupitia Wizara za Sekta ya elimu kutenga Bajeti kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule ya msingi na sekondari ili kuziandaa na utoaji wa Elimu kwa Mtaala mpya na matumizi ya teknolojia.

Vilevile HakiElimu imependekeza Serikali itenge Bajeti kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia vya teknolojia lakini pia kuanzisha vipindi vya ujuzi wa matumizi ya mtandao ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na umahiri wa kutumia mtandao kwa usahihi, uwezo wa kutatua matatizo na uwezo wa kujifunzia.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI.......USISAHAU KUSUBSCRIBE 

Post a Comment

0 Comments