Haydom Marathon 2024 kufanyika Mwezi Mei.Na John Walter-Manyara

Hospitali ya rufaa ya kilutheri Haydom imeanza mchakato wa kuandaa Mashindano makubwa ya Mbio za Nyika (HAYDOM MARATHON)  yanayotarajiwa kufanyika Mei 25,2024 mjini Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.

Katika mashindano hayo wananchi watapashwa kulipia shilingi elfu thelathini pekee (30,000) kwa ajili ya Usajili  kwa Kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5 pamoja kilomita 2 ambapo jumla ya shilingi Milioni 5 zinashindaniwa huku medali na tisheti zikitolewa kwa washiriki wote.

Akizungumzia mashindano hayo Mkurugenzi wa Hospitali ya Haydom Dr. Paschal Mdoe, amesema lengo kubwa la mashindano hayo ni kuimarisha afya za wananchi na kuwaaepusha na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

"Niwaombe wananchi wote bila kujali rika mjitokeze kwa wingi kujiandikisha "njoo tukimbie pamoja kwa ajili ya maisha" alisisitiza Mdoe

Mdoe amesema mbio za nyika ambazo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara katika tarafa ya Haydom zimekuwa na mafanikio makubwa ambapo  Hospitali imefanikiwa kujenga jengo la Mama na mtoto ambalo lipo mbioni kukamilika.

Aidha amebainisha kuwa fedha zitakazopatikana kwa mwaka huu kutoka kwa wananchi watakaochangia kwenye mbio hizo zitaelekezwa moja kwa moja kununua vifaa kwa ajili ya jengo hilo jipya.

Kauli mbiu ya Haydom Marathon mwaka 2024 inasema  "Ndio inawezekana, jiunge nasi".

Post a Comment

0 Comments