Madereva bodaboda waeleza walivyonufaika mafunzo ya usalama barabara

 


Na Mwandishi Wetu,Dodoma

BAADA ya Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kuanza kutoa mafunzo ya usalama barabarani awamu ya pili kwa madereva bodaboda jijini Dodoma , madereva hao wamekiri kunufaika na mafunzo hayo kwani kwa hivi sasa wanauelewa mkubwa kuhusu sheria za usalama barabarani.

Wameyaeleza hayo wakati wa kufanya tathimini kuhusu mafunzo hayo ambayo yamekuwa yakifanywa katika vijiwe vya bodaboda katika Jiji la Dodoma ambako Leo kijiwe cha bodaboda kinachojulikana Kijiwe Pesa kufanya tathimini kuhusu mafunzo hayo.

Wakizungumza na wakati wakitoa tathimini hiyo madereva bodaboda ambao wamepata mafunzo hayo wamesema mafunzo ya elimu ya usalama barabarani waliyoyapata yamewafumbua  macho na kuwafanya wawe na uelewa kuhusu sheria za barabarani.

Wamesema kabla ya mafunzo hayo walikuwa hawafahamu vizuri kuhusu Sheria za barabarani na changamoto kubwa kwa baadhi yao ilikuwa ni katika taa za barabarani kwani hawakuwa wanaelewa hata rangi za taa,hivyo walikuwa wanavuka hata wakikuta taa nyekundu,lakini sasa wanafahamu rangi zote za taa za kuongoza magari.

Dereva bodaboda Maulid Bakari amesema mafunzo ya usalama barabarani waliyoyapata yamekuwa na faida nyingi kwao na hasa ya kuelewa matumizi salama ya barabara na matokeo yake hata ajali zimepungua kwani wanafuata Sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake Amiri Matimba ambaye ni  Msaidizi wa Miradi kutoka Shirika la Amend Tanzania anasema wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa madereva bodaboda 47 kwa wiki ya kwanza jijini Dodoma.

Amesema wanaendelea kutoa mafunzo hayo katika vijiwe mbalimbali vya bodaboda huku akiwaomba madereva bodaboda kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo hayo yanayotolewa bure na Amend kwa kushirikiana na Uswisi.

Awali Mkufunzi wa Mafunzo hayo ambae pia ni Katibu wa Chama cha Walimu wa madereva Tanzania (CHAWATA) Massava Ponera akieleza tathimi ya mafunzo hayo toka walipoanza hadi walipofikia amesema mafunzo yanaendelea na madereva wengi wamefikiwa na mafunzo hayo.

"Kwa Dodoma hii ni awamu ya pili kutolewa kwa mafunzo hayo ambayo yamedhaminiwa na ubalozi wa Uswisi ili kuwezesha elimu ya usalama barabarani inafika kwa kundi la bodaboda ambalo jamii siku zote hulitazama kwa jicho la tofauti na kuamini ni wavunjaji wa sheria wakubwa."

Post a Comment

0 Comments