Mipira ya FIFA imefika halmashauri ya wilaya ya Babati.


Na John Walter-Babati
Halmashuri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara imepokea mipira 160 kutoka Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) itakayokwenda katika shule nne za msingi kwa lengo la kutekeleza programu za michezo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo Leo April 17,2024 iliyofanyika shule ya msingi Dareda kati,  Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo, amesema program za michezo mashuleni  ni muhimu kwa kuwa ni ajira na imewatoa watu wengi.

“Mipira hii ikafanye kazi iliyokusudiwa, msiifungie kabatini, tunataka, kuona vipaji vinaibuliwa kupitia mipira hii, muanzishe hata ligi ndani ya shule mkiwashirikisha na wasichana,” amesema Mbogo.

Aidha Mbogo  amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuthamini michezo mashuleni kwa vitendo.

Naye afisa Elimu Michezo wilaya ya Babati Meneja Byase, ameeleza kuwa jumla ya shule 4 kwa wilaya ya Babati  zitapatiwa mipira hiyo, ambapo kila shule imepangiwa kupata mipira 40 ambapo wanafunzi wataitumia wakati wa michezo.

Amewataka walimu kuhakikisha vipindi vya michezo mashuleni vinatumika kikamilifu na sio kutumia muda huo kufanya mambo mengine.
Byase amesema shirikisho la Soka Tanzania -TFF litakuwa likipita katika shule zote zilipokea mipira hiyo ili kuangalia Maendeleo na tija yake.

Kwa upande wake Kaimu Afisa elimu msingi wilaya ya Babati Joyce Uronu amesema mipira imetolewa shule ya msingi Gichameda, Migungani, Bashnet na Dareda kati.

Programu hiyo imeanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ikiwa ni mbadala wa programu ya grassroot ikiwa na lengo la  kukuza vipaji kwa wanafunzi.

Post a Comment

0 Comments