RC Sendiga: acheni kukwamisha miradi ya Maendeleo

Na John Walter -Hanang'

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amewataka wananchi kuipokea kwa mikono miwili miradi inayoletwa na serikali kwao kwa ajili ya maendeleo yao.

Sendiga amezungumza hayo kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa kata ya Endagaw wilayani Hanang', uliolenga kuwahimiza wenye maeneo eneo la mradi wa Skimu ya Umwagiliaji kupisha ili mradi huo uendelee kutekelezwa.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi  bilioni moja ulianza kutekelezwa kijijini hapo tangu mwaka 2016 lakini umekuwa ukisuasua kutokana na baadhi ya watu wachache waliogoma kupisha wakidai kupewa fidia.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa kwa mkuu wa mkoa, wananchi 108 wanadai fidia katika eneo ambalo lina hekari 26 ambapo ukigawanya kila mmoja anapata eneo lenye ukubwa wa mita  0.2.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, serikali inaendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kubuni na  kuanzisha Skimu za Umwagiliaji ili wakulima wafanye kilimo misimu yote hivyo inashangaza kuona wachache wasiotaka kuona hilo linafanyika.

Ameagiza viongozi wa kijiji waketi katika vikao vyao vya kisheria na kukubaliana ndani ya siku 30 ili fedha za mradi huo ziingie na kuanza kufanyiwa kazi kama ilivyo adhima ya serikali.

"Mimi nimekuja tuzungumze halafu niwaachie hili kwenye mikutano yenu ya vijiji, tuache maendeleo yafanyike, ni kwa faida yetu na vizazi vijavyo" alisema Sendiga

"Kule kulipojengwa skimu ya kwanza ndipo kwenye chanzo kikubwa cha maji kinachotoleza kulisha wilaya nzima ya Hanang'  ila watu wachache hao wamegoma kupisha hadi walipwe fidia ila mimi nimekuja kuwaomba mkubali ili mradi uendelee wakaati taratibu zingine zinaendelea kuwatafutia maeneo mengine ya kilimo"

Post a Comment

0 Comments