TAKUKURU Manyara yaokoa milioni 44 ndani ya miezi mitatu.

 


Na John Walter -Manyara

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) mkoa wa Manyara imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 44 katika oparesheni zake za uchunguzi na ufuatiliaji.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Manyara Suzana Raymond  amesema hayo ofisini kwake leo April 23,2024, mjini Babati alipokuwa akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo kwa kipindi cha januari hadi machi 2024  mbele ya waandishi wa habari.

Suzana alisema kupitia oparesheni, Shilingi Milioni 44,365,474 zimeokolewa kupitia ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Kiteto, Mbulu na ofisi ya mkoa ambapo Kati ya fedha hizo, shilingi 29,181,000 zilikuwa ni fedha ambazo zilikusanywa katika halmashauri ya wilaya ya Kiteto kupitia mashine za POS bila kuwasilishwa benki kwa muda mrefu kati ya miezi miwili hadi nane na baada ya ufuatiliaji fedha hizo zilipelekwa benki na hivyo kuzuia fedha hizo kutumika kinyume na taratibu.

Aidha katika ufuatiliaji ndani ya halmashauri ya wilaya ya Mbulu, taasisi hiyo ilifanikiwa kurejesha TRA  shilingi milioni 8,064,474 ambazo ni Kodi ya zuio.

Fedha zingine zilizookolewa na TAKUKURU mkoa wa Manyara ni kiasi cha shilingi milioni 7,120,000 ambazo ni mishahara ya mtumishi aliyeajiriwa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu.

Hata hivyo TAKUKURU mkoa wa Manyara kwa kipindi cha mwezi januari hadi machi 2024 imefuatilia  utekekezaji wa miradi ya Maendeleo 44 ya maji, afya, elimu na barabara inayogharimu shilingi Bilioni 13,025,684,439.

Post a Comment

0 Comments