V8 nyingine tena yakamatwa Babati ikisafirisha wahamiaji haramu.Na John Walter- Manyara
Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara April 07, 2024 wamethibitisha kuwakamata watu 17 raia kutoka nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila ya kufuata utaratibu ikiwemo kutokuwa na vibali.

Akizungumzia tukio hilo ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Lucas Mwakatundu amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Kijiji cha Kiongozi, Kata ya Maisaka, Tarafa ya Babati, Wilaya ya Babati, wakiwa wanasafirishwa kwenye gari aina ya V8 VXR yenye namba za usajili STL 1964.


Mwakatundu amewaomba wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Polisi katika kuhakikisha hakuna magendo yanayopitishwa kwa kutoa taarifa za watuhumiwa wa uhalifu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara pia limewaonya watanzania na wasio Watanzania kuacha kujihusisha na usafirishaji wa magendo ikiwemo wahamiaji haramu, dawa za kulevya na nyara za serikali.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni katika kizuizi cha Minjingu wilaya ya Babati mkoani Manyara, Jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 20 raia wa Ethiopia wakisafirishwa na gari aina ya Land Cruiser V8 YENYE bendera ya chama cha Mapinduzi.

Post a Comment

0 Comments