Wahanga mafuriko ya Rufiji wapatiwa msaada wa vyakula, majiko ya Gas na Oryx Gas, ASAS


KAMPUNI ya Oryx Gas Kwa kushirikiana na Kampuni ya ASAS wamekabidhi msaada wa vyakula pamoja na mitungi ya gesi ya oryx Kwa Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa Kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliopatwa na mafuriko wilayani Rufiji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Msaada huo uliotolewa na kukabidhiwa kwa Waziri Mchengerwa ni mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia vyenye thamani ya zaidi ya milioni 52 sambamba na  mitungi mikubwa 100 na majiko 100 pamoja na  mitungi midogo 100 yenye thamani ya zaidi ya mili 25.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo Waziri Mchengerwa amesema kwa niaba ya wananchi wanaushukuru kwa kupatiwa msaada huo ambao unakwenda kusaidia wananchi waliopatwa na mafuriko na kwa sasa wamehifadhiwa kambini kutokana na kukosa makazi pamoja na vyakula.


"Niko hapa kwa ajili ya kupokea msaada kama tunavyofahamu hali ya  Rufiji kila mmoja wenu anatambua kwamba mwaka huu mafuriko yamekuwa makubwa kupita kiasi,tunayafananisha mafuriko ya mwaka huu kama mafuriko yaliyotokea mwaka 1972 na mwaka 1974 ambapo Baba wa Taifa alilazimika yeye pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wakati huo mzee Rashid Mfaume Kaka kwenda Rufiji wao kwa pamoja kuzunguka na kutoa pole kwa wananchi wa Rufiji

"Na leo tunaashuhudia kwa muamko wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ni mfariji namba moja katika Taifa letu alioutoa kwa siku ya jana alipokuwa kule Arusha lakini taarifa ambazo amekuwa akizitoa kuwataka Watanzania kuwa wamoja na kusaidia wale ambao wana nafasi basi wajitolee kwa ajili ya wenzao,"amesema.

Ameongeza kuwa hivyo leo wanashuhudia shehena ya vyakula ambavyo vimetolewa na ASAS pamoja na Kampuni ya Oryx Gas ambapo Oryx wametoa mitungi pamoja na majiko ambayo wananchi wa Rufiji hasa walioko makambini watakwenda kutumia.


Pia Oryx kwa kushirikiana na ASAS wametoa vyakula ambavyo vitakwenda kutolewa kwa wananchi wote walioko makambini ambao wanahifadhiwa na wanahudumiwa na Serikali kwa wakati huu huku akitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwani tayari amekwisha elekeza  utolewaji wa shehena ya vyakula

Ametaja vyakula hivyo ni  mchele  Maharage, unga pamoja na vyakula  vingine ambavyo Rais Dk Samia ameelekeza kwenda Rufiji kwa ajili ya kusaidia wananchi waliokumbwa na mafuriko kwa mwaka huu.

"Niendelee kuwasihi Watanzania wote katika maeneo yao wale wenye nafasi wanaona wanataka kutoa kwa ajili ya ndugu zao tunawakaribisha Rufiji.Nitume nafasi hii kuwashukuru na kuwaomba tuendelee kushikamana katika kipindi hiki kugumu, tuendelee kuwa wamoja na kwamba mafuriko hayo hayakuanza mwaka huu yamekuwepo tangu enzi wa baba wa Taifa."

Waziri Mchengerwa ameeleza pia kama Serikali imekwisha andaa mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu ambapo mpangowa muda mfupi ni kwenda kuhakikisha kaya zote ambazo zimeathirika zinapata msaada na wale ambao hawana pakukaa yapo maeneo ya Serikali ambayo yametengwa na watakaa hapo.

Pia wale ambao wamepata mahali pakukaa Serikali itaangalia namna gani iweze kuwasaidia hasa katika eneo la mbegu na katika hilo watapanga na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa ajili ya kuhakikisha mbegu inatolewa kwa wananchi hao.

"Tayari tumeshatoa mchango wa takribani milioni 50 kusaidia kununua vitu kama mbegu baada ya mafuriko  lakini Wizara ya Kilimo haiko nyuma Husein Bashe ameniahidi atafika Rufiji kuona cha kufanya ikiwemo kutafuta mbegu kwa ajili ya wananchi wa Rufiji.Tunawashukuru Oryx Gas na ASAS kwa msaada ambao wameutoa kwa ajili ya wananchi wa Rufiji.

Awali kabla ya kukabidhi msaada huo, Meneja Mauzo wa Oryx Gas Shaban Fundi  amesema kwa niaba ya  Oryx Energies wanatoa pole kwa waathirika wote wa mafuriko yaliyotokea nchini hususan watu wa Rufiji.

"Kampuni ya Oryx Gas ikishirikiana na wadau wenzetu ASAS tumeamua tuwashike mkono wenzetu wa Rufiji kwa kuwapa msaada wa vyakula na mitungi ya gas ili kusaidia watu waliopo katika makambi ya kutolea misaada ya kibinaadam.

"Tumetoa mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya milioni 52. Zaidi tumetoa mitungi mikunwa 100 na majiko 100, pia tumetoa mitungi midogo 100 yenye thamani ya zaidi ya mili 25.Tunampa pole muheshimiwa Waziri Mchengerwa, Wananchi wa Rufiji na Serikali kwa ujumla,"amesema Fundi.

Post a Comment

0 Comments