Walawiti na wabakaji watoto kukiona -Sillo


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) amewataka wale wote wanaotafuta utajiri kwa dhana potofu ya kulawiti na ubakaji watoto kuacha mara moja kwani Serikali na Vyombo vya Ulinzi na Usalama havitokuwa na muhali na mtu yoyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.

Akizungumza Aprili 14, 2024 katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) lililopo Mtaa wa Nar Usharika wa Qaloda Dayosisi ya Mbulu Wilayani Babati Mkoani Manyara,  Mhe. Sillo alisema kuwa, kuna mambo mengi ya kikatili yanayofanyika ambayo yanalenga kuwapatia utajiri baadhi ya watu hivyo nitumie fursa hii kutuma salamu kuwa sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Vyombo vyetu tutapambana kuhakikisha tunatokomeza viashiria vyote na kukamata wahalifu.

"Viongozi wa Dini katika mahubiri yenu muwaeleze waumini kuwa hakuna utajiri unaopatikana kwa njia ya kufanya ukatili hivyo Baba Askofu nikupongeze ila uzidi kutoa mafundisho kuwa utajiri wa halali na wa amani unapatikana kwa kufanya kazi ambayo haivunji sheria na taratibu za nchi pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu pia kwa kuwa mimi ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nimeshaelekeza Vyombo ambavyo vinafanyakazi chini ya Wizara yangu kuendelea na msako kwa lengo la kudhibiti na kuwakamata wahalifu hao" Alisema Mhe. Sillo.

Katika hafla hiyo jumla ya shilingi 29,435,000.00 zilikusanywa huku ahadi zikiwa shilingi 7,170,000.00 ambapo inafanya jumla ya shilingi 36,652,000.00 kwa ajili ya uendelezwaji wa Ujenzi wa Kanisa hilo.

Kwa upande wake Mhe. Baba Askofu Nicholas Nsanganzelu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu alimshukuru Naibu Waziri Mhe. Sillo kwa mchango wake na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo ambayo yatapelekea ujenzi wa nchi bora na kupunguza ukatili.

"Nikuhakikishie tu Mhe. Naibu Waziri kuwa sisi kama Kanisani na Wananchi wa Kitongoji hiki hatuwezi kufumbia macho viashiria au matukio yoyote ya ukatili tunaungana na serikali kupiga vita mambo hayo" Alisema Mhe. Baba Askofu Nsanganzelu

Nao baadhi waumini walioshiriki hafla hiyo wamebainisha kuwa, watatumia maelekezo na mafundisho yaliyotolewa siku hii ya leo kuendelea kusimamia vema malezi ya watoto na kutoa taarifa kwa Serikali kuhusu ukatili wowote utakaojitokeza katika jamii zao.

Post a Comment

0 Comments