Wananchi walalamika ndugu zao kupotelea hifadhini Tarangire.


Na John Walter-Babati

Wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi ya taifa ya Tarangire wilayani Babati mkoani Manyara, wamelalamikia baadhi ya ndugu zao kupotea pindi wanapoingia katika hifadhi hiyo na kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo.

Wamedai kuwa wanyamapori wanapowavamia wanatoa taarifa kwa mamlaka husika ili warudishwe lakini wao wanapowakamata wanawatesa bila hata kuwajulisha ndugu zao.

Wametoa kilio hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Endagile kata ya Mamire ulioitishwa na mkuu wa wilaya Lazaro Twange kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa kata ya Mamire.

Akijibu hoja hiyo Afisa mhifadhi Tarangire Fabian Nyakoro anasema hawana taarifa juu ya kukamatwa au kushikiliwa kwa watu ndani ya hifadhi kwa kuwa hawana mahabusu na kwamba wanapokamatwa walioimgia kinyume cha sheria wanawafikisha katika vyombo vya sheria ikiwemo jeshi la polisi kwa ajili ya taratibu zingine.

"Huwa baada ya kuwakamata tunawapeleka sehemu inayostahili ambayo ni polisi, kiukweli hifadhini sio sehemu salama, kuna wanyama wakali, hifadhi hautwezi kumkamata mtu na kumfanyia kitu kibaya" alisema Nyakoro

Ametoa rahi kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi kufanya kazi halali za kuwaingizia kipato na sio kufanya shughuli ndani ya hifadhi kwa kuwa sio salama.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amekiri kupokea malalamiko ya kupotea kwa wananchi katika hifadhi hiyo na kutoa rahi kwa mamlaka kulichukulia kwa uzito suala hilo na kudumisha mahusiano mema na wananchi wanaopakana na hifadhi.

"Kakaeni huko kwenye vikao vyenu huu mchezo muachane nao, mtu akikosea mumkamate mumfikishe kwenye vyombo vya sheria na kutoa taarifa kwa viongozi wao, na hizi sio taarifa za kutungwa ni za kweli, wanaingia huko kuvua samaki, wanajua hadi mabwawa yalipo na siku zingine mnawauzia ila wakija huko mnawakamata" alisema Twange

Hata hivyo changamoto ya uvamizi ya wanyamapori katika makazi ya watu wanaoishi pembezoni mwa hifadhi limekuwa suala la kujirudia  mara kwa mara hivyo serikali na wataalamu wanapaswa kubuni njia itakayozuia na kuwadhibiti wanyama hao ili kuendelea kuwepo kwa hifadhi hiyo na usalama wa wananchi.

Kwa upande wake afisa Wanyamapori wilaya ya Babati Christopher Laizer amesema serikali ipo kwenye mchakato wa kuwalipa fidia wananchi walioharibiwa mazao yao na wanyamapori katika vijiji vinavyopakana na hifadhi.

Post a Comment

0 Comments