ECLAT na UPENDO kujenga chuo cha Vijana wa kike Simanjiro.



Na John Walter-Manyara

Katika kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali, wadau wa Maendeleo Shirika lisilo la kiserikali linalojiuhusisha na masuala ya elimu -ECLAT Development Foundation wameanza ujenzi wa chuo cha Mafunzo,ujuzi na malezi kwa wasichana wanaotoka katika mazingira magumu.

Jiwe la msingi la Ujenzi wa Chuo hicho kinachojengwa Kijiji cha Emboreet wilayani Simanjiro,  limewekwa na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga Mei 17,2024.

Mkurugenzi wa Shirika hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Mheshimiwa Peter Toima amesema wanafanya kazi za Maendeleo katika mikoa sita nchini kwenye Miradi ya elimu, Maji, Afya na uwezeshaji makundi ya Vijana na Wanawake.

Hadi sasa Shirika hilo la Maendeleo limeshachangia zaidi ya shilingi Bilioni 25 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo wilayani Simanjiro.



Toima amesema wamejenga zaidi ya shule 50 huku asilimia kubwa zikiwa mkoa wa Manyara, vikundi 75 vya Wanawake ambapo asilimia 79 ya vikundi hivyo vipo mkoani Manyara.

Amesema yote hayo yamewezekana kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya awamu ya sita ya chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kushirikiana vizuri  na wadau wa Maendeleo.

Aidha wafadhili wa Mradi huo ECLAT Development Foundation ya Tanzania na Upendo Foundation ya nchini Ujerumani,  wamesema Fedha kwa ajili ya mradi huo zipo na kwamba Ujenzi utaanza mei 18,2024.



Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho, amesema Serikali itaendelea kuweka Mazingira rafiki kwa wawekezaji wote katika juhudi zao ambazo wanazifanya kuunga mkono utekekezaji wa masuala mbalimbali ya Maendeleo.

"Naomba niwaahidi kwamba sisi serikali kazi yetu kubwa ni kutengeneza mazingira rafiki ya kuwafanya wadau wetu mbalimbali wanapokuja waweze kufanya shughuli zao vizuri kwa sababu wanufaika wa miradi hii ni Watanzania" alisema Sendiga

Ezekiel Lesenga Diwani kata ya Leiborisiret  amelishukuru Shirika la ECLAT kwa kujenga shule nane katika kata yake.

Post a Comment

0 Comments