NIMR yapongezwa kwa ushawishi wa utafiti kimataifa


NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu na mchango wa utafiti wa kisayansi katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisayansi zinazochangia kuchochea maendeleo ya nchi.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Mei 14, 2024 jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika ufunguzi wa Mkutano wa 32 wa Masuala ya Utafiti wa Kisayansi  ulioandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

‘‘Serikali inayoongozwa na Rais Samia inaamini katika tafiti za kisayansi na inaamini pia kuwa hakuna maendeleo bila utafiti na hivyo ili kupata mafanikio ni lazima tufanye utafiti’’, amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza ‘‘Kama mnavyofahamu kupata maendeleo ya mahali popote ili matokeo yaonekane lazima kuwe na utafiti wa kisayansi na uweze kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali kwa hivyo maendeleo yoyote bila utafiti yatakuwa ni maendeleo ya kubahatisha, na kama ni ya kubahatisha kutakuwa na kukosea kungwi matokeo yake kutakuwa na matumizi ya rasilimali nyingi zaidi kabla ya kupata jibu sahihi jambo ambalo lingeepukika, hivyo wataalamu hawa wako hapa  kujadili tafiti mbalimbali katika sekta ya afya  mfano chanjo’’.

Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya na itaendelea kuunga mkono tafiti za kisayansi huku akiziasa taasisi za utafiti kushirikiana katika tafiti kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali ili kuchangia maendeleo ya nchi.

Ameongeza kuwa taasisi hizo zinapaswa kuhamasisha wananchi kutumia matokeo ya utafiti katika kufanya maamuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Sambamba na hilo, Dkt. Biteko amesema  Serikali  imewekeza vya kutosha kwenye utafiti katika sekta ya afya ili kuwa na ugunduzi wa ndani ya nchi akiongeza kuwa pamoja umuhimu wa watafiti  kutoka nje kuna umuhimu wa kuwa wagunduzi wa ndani.

 Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kutoa kipaumbele katika masuala ya utafiti kwa lengo la kuwajengea uwezo watafiti wa ndani ya nchi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohitaji utafiti wa kisayansi mara zitakapotokea.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi kupitia tafiti zake mbalimbali inazofanya akitolea mfano ugunduzi wa dozi moja ya chanjo ya mlango wa kizazi uliofanywa na NIMR mkoani Mwanza.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiendesha makongamano kwa kushirikiana na wadau ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sera za afya pamoja na kufanya maamuzi yanayosaidia kuboresha sekta hiyo nchini.

Awali, Dkt. Biteko ametembelea mabanda ya vifaa vya maabara vya kupima magonjwa mbalimbali ikwemo kifua kikuu, malaria na tafiti za dawa za asili.

Post a Comment

0 Comments