RC Manyara awaonya wenye tabia ya kutelekeza Familia.Na John Walter Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga, amewaonya wanaume wenye tabia ya kutelekeza familia zao na kumuachia mama pekee mzigo wa kulea mtoto/ watoto na kuwataka kuacha mara moja.

Sendiga amesema familia bora inaundwa na Mama, Baba na watoto hivyo ni lazima kila mmoja atumize wajibu huo bila kumtegea mwenzake.

Ametoa wito huo leo Mei 14,2024 mjini Babati ikiwa Dunia  inaelekea kuadhimisha siku ya Familia kesho mei 15, ambapo katika mkoa wa Manyara Maadhimisho hayo yatafanyika katika Kijiji cha Magugu wilayani Babati yakiongozwa na  kaulimbiu isemayo   "TUKUBALI TOFAUTI ZETU KWENYE FAMILIA, IMARISHA MALEZI KWA WATOTO".

Siku hiyo ya familia ni mahususi kwa ajili ya kuikumbusha taasisi hiyo muhimu majukumu yake ili iweze kuyatimiza ipasavyo kwa kuwa ndo msingi wa kila jambo.

Amesema familia yeyote ina jukumu la kuhakikisha inatoa huduma muhimu za kimsingi ikiwemo chakula,malazi,mavazi, Afya, elimu na ulinzi.

Tafiti zinaonesha kuwa migogoro katika familia, ulevi wa kupindukia, baba kuwa na Wanawake wengi na kushindwa kuwahudumia ndo chanzo cha maisha duni kwa watoto na tabia zisizofaa kwa jamii.

Aidha kutokuwa na uangalizi mzuri kwa watoto haswa wa kike kunasababisha kuingia mapema katika vitendo vya ngono wakiwa katika umri mdogo mwishowe kupata mimba za utotoni na kushindwa kuendelea na Masomo.

Pia kukosekana kwa malezi bora na uangalizi, watoto wa kiume huingia kwenye masuala ya ulevi, matumizi ya dawa za kulevya, wizi, ushoga.

Utafiti unaonesha kuwa asilimia 22 ya watoto wenye umri kati ya Miaka 15-19 wanapata ujauzito wakiwa katika umri mdogo ukilinganisha na asilimia 27 ya watoto wenye umri huohuo ambao mwaka 2015-2016 ilionyesha kwamba kiwango cha mimba za utotoni haswa vijijini kimekuwa hadi kufikia asilimia 21 na kwa mijini asilimia 16.

Post a Comment

0 Comments