F Baba Mzazi na Paroko msaidizi wakamatwa mauaji ya Asimwe | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Baba Mzazi na Paroko msaidizi wakamatwa mauaji ya Asimwe


Jeshi la Polisi linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la mauaji ya mtoto aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino), Asimwe Novart mwenye umri wa miaka miwili na nusu.

Mtoto huyo aliporwa na watu wasiofahamika kutoka kwa mama yake Mei 30, 2024 katika kijiji cha Bulamula Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Mwili wa mtoto huyo ulipatikana Juni 17, 2024 ukiwa hauna baadhi ya viungo katika kijiji cha Makongora.

Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imeeleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema walianza msako mkali kuanzia Mei 31, 2024 hadi usiku wa kuamkia leo Juni 19, 2024 ambapo watuhumiwa tisa wamekamatwa wakiwa na viungo vinavyodhaniwa ni vya mtoto Asimwe Novart wakitafuta mteja.

Watuhumiwa waliokamatwa ambao kwa mujibu wa polisi wameeleza jinsi walivyoshiriki katika tukio hili ni pamoja baba mzazi wa mtoto huyo, Novart Venant.

Wengine ni Desideli Evarist ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Nyakahama na Elipidius Rwegoshora, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika ambaye anadaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto huyo wafanye biashara ya viungo vya binadamu.

Paroko huyo msaidizi anatuhumiwa pia kwamba ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.

Watuhumiwa wengine ni Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara, Faswiru Athuman mkazi wa Nyakahama, Gozibert Alkadi wa Nyakahama Kamachumu, Rwenyagira Burka wa Nyakahama Kamachumu, Ramadhani Selestine wa Kamachumu na Nurdin Hamada ambaye pia ni mkazi wa Kamachumu.

Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa watu wanaoendekeza imani za kishirikina ikiwemo kupiga ramli chonganishi wakiaminishana kwamba wanaweza kupata utajiri kwa njia za kishirikina kuacha tabia hizo.

"Watu waache kudanganyana kwamba kuna utajiri unaopatikana kwa kumiliki viungo vya binadamu mwenye ualbino, si kweli kwa sababu kama ingekuwa hivyo familia zenye watoto au ndugu wenye ualbino wangekuwa na utajiri mkubwa," amesema Misime.

Post a Comment

0 Comments