Dkt. Biteko ateta na viongozi wa CCM Bukombe


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa uimara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatokana na misingi iliyowekwa na waasisi ya kushirikisha wanachama wake kutoka ngazi ya balozi, kata hadi wilaya.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Juni 9, 2024  katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita wakati akihutubia mkutano wa mabalozi, viongozi wa CCM ngazi ya matawi na mashina  ya Wilaya ya Bukombe.

Ametaja lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi hao wa CCM kuwa ni kufanya tathmini ya hali ya maendeleo wilayani hapo na umuhimu wa maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu.

‘’Tukisema CCM ni imara, uimara wake unaanzia kwenye ushirikishwaji wa wanachama kuanzia ngazi za chini jambo linalo tuwezesha kung’amua na kuzishughulikia changamoto za wananchi kwa wakati na kuwaletea maendeleo’’, amesema Dkt. Biteko


Amebainisha kuwa uimara wa CCM ni matokeo ya mfumo wake unaoanzia ngazi ya chini kwenye shina na kuwa mabalozi ni kiungo muhimu kwa ustawi wa chama hicho na kamwe wasijione wadogo.

Aidha, Dkt. Biteko amesisitiza  kuwa ni muhimu mabalozi hao  kuwa imara ili kusimamia vema utekelezaji wa ilani ya CCM katika maeneo yao na uimara wao kwa kushirikiana na wenyeviti ndio mafanikio ya CCM na Taifa kwa ujumla.

Vilevile, Dkt. Biteko amewataka mabalozi na watendaji kuwaunga mkono madiwani ili wafanye kazi kwa umoja  na kwa maslahi ya ustawi wa wilaya yao kwani kazi zilizofanywa na madiwani kwenye kata ni nyingi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.

Pamoja na hayo amemtaka kila diwani kwenye kata yake kuitisha mkutano mkuu wa kata kueleza  ili kueleza wananchi mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao. Sambamba na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, afya, barabara na shule katika Wilaya ya Bukombe.

Kuhusu maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Dkt. Biteko amesema “ Tamaa yangu ni kuona tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa itakapofanyika, Bukombe inakuwa  ya kwanza na ya mfano kwenye kura za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kufikia hili ni muhimu kwa pamoja kuendelea na jitihada za kuimarisha chama chetu”.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Ndugu Nicholous Kasendemila  amesema kuwa mabalozi hao 729 wanaowakilisha kata 17 zilizopo katika Wilaya ya Bukombe ni watu muhimu katika kuimairisha Chama Cha Mapinduzi katika wilaya hiyo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wilayani humo  pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella.

Post a Comment

0 Comments