JKT yatoa nyongeza ya muda kwa vijana waliohitimu kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria

 


Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa nyongeza ya awamu ya pili ya majina ya vijana waliohitimu kidato cha sita kwa mwaka 2024 kujiunga na mafunzo ya JKT na vijana hao watatakiwa kujiunga katika makambi yaliyojirani na wanapoishi huku likiwakata vijana wote walioitwa awamu ya kwanza ambao hawajaripoti makambini mpaka sasa waripoti mara moja katika makambi yaliyo karibu na makazi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kuwa wametoa nyongeza ya awamu ya pili ya majina ya vijana waliohitimu elimu ya Kidato cha Sita mwaka 2024 kujiunga na Jeshi hilo ili kufanya mafunzo hayo ya lazima.

“Orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo awamu ya pili na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz”,amesema.

Ameongeza, “Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa hivi karibuni alitoa wito kwa vijana wahitimu wa elimu ya kidato cha Sita mwaka 2024 kujiunga na mafunzo ya JKT kwa lazima (mujibu wa sheria) kwa mwaka 2024, vijana hao walitakiwa kuripoti makambi ya JKT walipopangiwa kuanzia Juni 1,2024 hadi Juni 7,2024 wakiwa na vifaa vilivyoainishwa na JKT kuripoti navyo makambini.

Aidha ameongeza kuwa vijana wote ambao hawajaripoti wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia leo Juni 22,2024 hadi Juni 26,2024.

Amesema Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana waliohitimu kidato cha Sita mwaka huu kuungana na vijana wenzao ili kujengewa uzaIendo, umoja na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa lao.

 

Katika hatua nyingine amesema JKT imeamua kuchukua uamuzi wa kuongeza awamu ya pili ya kuwaita vijana wa kwa mujibu wa sheria baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwa wazazi na walezi kutokana na kupangiwa mbali na maeneo walipo.

 

Amesema serikali inaendelea kuiwezesha JKT katika rasilimali fedha ili kuongeza miondombinu ya kuweza kuhudumia vijana wengi zaidi kufaidika mafunzo hayo.

 

Post a Comment

0 Comments