F Kamanda wa polisi Manyara agawa bima za afya kwa wasiojiweza. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kamanda wa polisi Manyara agawa bima za afya kwa wasiojiweza.


Na John Walter -Manyara

Kazi ya Jeshi la polisi ni kulinda raia na na mali zake, lakini Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, SACP George Katabazi ameenda mbali zaidi na kulinda afya za wananchi kwa kugawa kadi za bima ya afya (ICHF) kwa makundi ya wazee, wajane, wenye ulemavu na wanaoishi katika Mazingira magumu.

Kamanda Katabazi amesema baadhi ya wananchi hawana uwezo wa kupata huduma za afya hivyo ili kupunguza changamoto hiyo ameona ni vyema atoe bima hizo ili kuwasaidia wananchi wake wawe salama kiafya.

"Tunatoa hizi  bima kwa sababu ya usalama wa afya, usalama wa afya ni muhimu sana kwa sababu unatusaidia jeshi la polisi kuweza kutekeleza majukumu yake kwa kuwa mwananchi akiwa na afya bora ataweza kushiriki kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu" alisema Katabazi

Katabazi amesema ameamua kuunga  mkono jitihada za serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watu wanakuwa salama kiafya ili kuweza kuwa na Maendeleo.



Afisa mwandikishaji wa Bima ya Afya ICHF iliyoboreshwa Elibarick Michael, amesema zoezi hilo limeanza Februari mwaka huu ambapo hadi sasa wameshawaandikisha Wanufaika zaidi ya 160 katika wilaya za Babati, Mbulu na Hanang'  na  kabla mwaka haujaisha watawafikia wananchi wenye mahitaji maalum katika wilaya za Simanjiro na Kiteto.



Michael amesema bima ya afya ya ICHF iliyoboreshwa inapokelewa katika vituo vya serikali Zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya hadi za rufaa.

Aidha wananchi wa wilaya za Mbulu, Babati na Hanang' walionufaika na bima hizo wamemshukuru Kamanda kwa msaada huo wakimuombea baraka kwa Mungu.



Mwenyekiti wa Kijiji cha Ming'enyi Kata ya Gehandu wilaya ya Hanang'  Karani Tlatla, amesema alichokifanya Katabazi ni cha kuungwa mkono na watu wengine wenye mapenzi mema kwa kuwa zipo kaya nyingi ambazo hazina hata uwezo wa kujigharamia matibabu kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji cha Nangwa wilaya ya Hanang'  Stephano Kitila, amemshukuru Kamanda Katabazi kwa kuona mbele na kutoa kadi hizo kwa kuwa uhitaji ni mkubwa kwa kuwa watu wengi hawana uwezo wa kifedha.

Afisa mtendaji wa mtaa wa Ayamaami wilaya ya Mbulu Everest Mwitewe, amesema katika mtaa wake kaya 5 zenye watu 30 wasio na uwezo ambao pia wanahudumiwa na serikali kupitia Mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wamepatiwa bima za Afya.

Post a Comment

0 Comments