Naibu waziri Sillo awajulia hali majeruhi wa ajali Mbeya.



Na Mwandishi wetu-Mbeya

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) Juni 7, 2024 amefika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya iliyopo Jijini Mbeya kuwajulia hali na kuwapa pole majeruhi wa ajali iliyotokea Juni 5 katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela na kusababisha vifo vya watu 15 na  majeruhi kadhaa.

Akizungumza baada ya kuwajulia hali na kuwapa pole majeruhi hao Mhe. Sillo alimpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha Hospitali za Rufaa na kuzipatia vitendea kazi.

"Tumeona majeruhi wamehudumiwa vizuri na kupatiwa vipimo vyote kwa wakati, na hata ndugu zetu waliopoteza maisha wamehifadhiwa vizuri tumpongeze Mhe. Rais," alisema Mhe. Naibu Waziri


Aidha alivipongeza Vyombo vya Usalama na Wananchi kwa namna walivyowahi eneo la tukio kusaidia kuokoa watu waliokuwa katika ajali hiyo na kutoa Rai kwa Wananchi wasio waaminifu kuacha tabia za udokozi pindi wenzao wanapopatwa na madhira kama hayo. 

Pia alielekeza Kikosi cha Usalama barabarani nchini kusimamia vyema sheria za barabarani na kuchukua hatua kali kwa madereva wanaokiuka sheria na kutozingatia alama zilizowekwa barabarani. 


"Kama ambavyo bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi ilivyoeleza na Waziri wetu Mhe. Mhandisi Hamad Masauni tupo katika mchakato wa kuanza ukaguzi wa magari kwa kutumia mitambo ya kisasa,  hivyo wakati tukisubiri mpango huo wamiliki wa vyombo vyote vya moto wafanye matengenezo ya mara kwa mara," alisema Mhe. Sillo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, DCP Ramadhan Ng’anzi alisema kuwa amepokea maelekezo na wanaenda kwenye utekelezaji ndani ya siku 14 wataanza majaribio ya kupima magari kwa mitambo ya kisasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya ambapo alisisitiza kuwa madereva ambao watakiuka utaratibu watafungiwa leseni zao.

Aidha Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji alisema kuwa hadi sasa kuna mwili mmoja ambao haujatambuliwa ila majeruhi wawili tayari wameruhusiwa baada ya afya zao kuridhisha.


Post a Comment

0 Comments