Waendesha pikipiki zaidi ya 180 wapatiwa mafunzo Kilindi

 


Na Mwandishi Wetu, Kilindi

VIJANA zaidi ya 180 wanaoendesha pikipipiki katika Wilaya ya Kilindi moani Tanga wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani kwa lengo la kuwawezesha kufahamu sheria ili kupunguza ajali za barabarani.

Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Shirika la Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswiss nchini Tanzania yamefanyika katika vituo vinne vya Songe Mjini, Kwa Madoti, Kibirashi na KwediBoma ambapo vijana hao wamepata mafunzo ya usalama barabarani pamoja na mafunzo ya huduma ya kwanza.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga Hashim Mgandilwa amesema yamekuja wakati muafaka kwani waendesha bodaboda wengi katika Wilaya hiyo hawana elimu ya usalama barabarani na hivyo baadhi yao kuwa chanzo cha ajali za barabarani.

“Tumekuwa na mipango mbalimbali kuhakikisha tunatoa elimu ya usalama barabarani kwa kundi la vijana na hasa waendesha bodaboda, hivyo kwa kushirikiana na Chuo cha VETA Wilaya ya Kilindi tulifanikisha vijana 100 kupata mafunzo .

“Tunashukuru leo Amend wamekuja Kilindi kwa ajili ya kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa vijana wetu, tunaamini mafunzo haya yatasaidia vijana kufahamu sheria za usalama barabarani na kuzifuata ili kwa pamoja tupunguze ajali za barabarani.Tunawaomba Amend waendelee na mafunzo haya kwani mahitaji ni makubwa,”amesema Mgandilwa.

Kwa upande wake Mratibu wa Amend Tanzania Ramadhan Nyanza amesema katika muendelezo wa kampeni yao ya kutoa mafunzo ya usalama barabarani hatimaye imewafikia vijana wa Kilindi na 180 wameshiriki mafunzo hayo.

Amesema Amend katika kufanikisha mafunzo hayo wamekuwa wakishirikiana na wadau muhimu kama Jeshi la Polisi pamoja na Msalaba Mwekundu.

“Katika muendelezo wa kampeni za usalama barabarani,Shirika la Amend kupitia Ubalozi wa Uswiss Tanzania kwenye Mradi wa Usalama wa pikipiki kwa kundi la Vijana Tanzania tumeendelea na kampeni hii katika Mkoa wa Tanga na leo tuko Kilindi,”amesema Nyanza.

Post a Comment

0 Comments