Wafanyabiashara Manyara walia na utitiri wa kodi na tozo.Na John Walter -Manyara

Wafanyabishara wa Mkoa wa Manyara wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza mrundikano wa tozo na kodi mbalimbali zinazotozwa kwa sasa hali itakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa tija.

Wametoa ombi hilo mbele ya Rais wa Chemba ya wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo (TCCIA) Mheshimiwa Vicent Minja alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kikazi iliyolenga kusikiliza kero za wafanyabiashara na fursa zilizopo mkoani Manyara.

Aidha baadhi ya wafanyabiashara wamedai mamlaka ya Mapato TRA imekuwa ikiwafungia akaunti zao za benki.

Pia Mheshimiwa Vicent Minja ametoa mapendekezo kwa serikali kuanzisha tume ya kikodi.

"Tume ya Mwisho ilianzishwa mwaka 1998 zaidi ya miaka 26, mambo kwa sasa yamebadilika Sana, kumeanzishwa tozo nyingi sana na authority nyingi ambazo kila moja ina tozo na faini, hakuna mfanyabiashara anayeweza kuendelea na biashara endapo atalipa tozo na Kodi zote" alisema Minja 

"Namaliza ziara yangu leo Manyara, wiki inayofuata tunafanya kazi ya kuchambua hizi changamoto na kuandika taarifa ya nchi nzima ambapo tutafanya engagement na Serikali " alisema Vicent 

Amesema TCCIA wataandika mapendekezo hayo na kuyawasilisha serikalini ili kuangalia namna ya kuboresha baadhi ya sheria kwa ajili ya marekebisho lengo ni kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki.

Rais wa Chemba ya wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) Vicent Minja amefanya ziara katika mikoa 26 kujua uhai wa Chemba, kuangalia mahusiano ya Chemba na wadau wengine, kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na fursa zilizopo kwenye mikoa hiyo.

Post a Comment

0 Comments