F Walimu na wajasiriamali Lindi waishukuru TRA. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Walimu na wajasiriamali Lindi waishukuru TRA.

 



Na Ahmad Mmow, Lindi.


Baadhi ya walimu na wafanyabiashara  mkoani Lindi wameishukuru mamlaka ya mapato (TRA) mkoani Lindi kwa kuendelea kuwapa elimu ya biashara na ulipaji kodi ya mapato.


Jana wakizungumza mjini Lindi wakati wa semina ya wafanyabiasha, wakandarasi na wazabuni ambayo iliandaliwa na TRA na kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwalimu Frank Kapinga wa shule ya sekondari ya Lindi na Mrita Amidu Kangomba mjasiriamali katika manispaa ya Lindi walisema semina hiyo ya siku moja imewasaidia kuelewa mambo ambayo kabla walikuwa hawajui. Ikiwamo kujua fedha zinazotumika katika miradi na mishahara ya watumishi inatoka wapi. Lakini pia faida za kupambana na rushwa.


Mwalimu Kapinga kwa upande wake alisema kabla ya semina hiyo baadhi yao walikuwa hawajui fedha zinazotumika kulipa mishahara ya watumishi na zinazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo zinapatanaje. Hata hivyo baada ya semina hiyo wamejua njia na namna zinavyokusanywa na kupelekwa hazina kuu.


Aidha Mwalimu huyo wa shule ya sekondari ya Lindi alisema kupitia semina hiyo wameweza kujua madhara ya rushwa, umuhimu wa kupambana nayo na jinsi ya kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali.


Alibainisha kwamba  kabla ya semina hiyo wengi wao ingawa shule zao zinapelekewa fedha lakini walikuwa hawajui jinsi ya kusimamia na kuzuia zitumike vibaya. Kwani walio wengi hawana taaluma ya manunuzi na uhasibu.


Mwalimu huyo aliahidi kwa kushirikiana na walimu wenzake walioshiriki semina hiyo watakuwa mabalozi wazuri. Nakwamba miradi na fedha za miradi hiyo zitasimamiwa vizuri.


Nae mjasiriamali Mrita Amidu Kangomba alisema elimu waliyopata imeweza kuwafanya wajue madhumuni na malengo ya TRA ya kukusanya kodi na umuhimu wa kila mfanya biashara kulipa kodi.


" Nime baini kunahitajika utaratibu wa utunzaji mzuri wa kumbu kumbu na kutoa resiti kila tunapouza bidhaa. Kwani tusipo fanya hivyo tutakuwa tumeshiriki kukwamisha maendeleo," alisema Kangomba.


Mjasiriamali huyo nae amesema kwamba anatambua wasipotambua, kujipanga na kushiriki kikamilifu  mapambano dhidi ya rushwa watakuwa wameshiriki kukwamisha nia njema ya serikali ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.


Kwa upande wake mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Lindi, Asha Kwariko alisema lengo la semina hiyo iliyoandaliwa na TRA na kuishirikisha taasisi hiyo kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa, wajibu wa wadau kushiriki mapambano dhidi ya rushwa na wajibu wa kulipa kodi.

Post a Comment

0 Comments