Wananchi 114 wapatiwa bima za afya bure na Taasisi ya Kumbilamoto Foundation


TAASISI ya Kumbilamoto Foundation imegawa bima za afya bure kwa kaya 19 zenye jumla ya watu 114 katika kata ya Vingunguti wilayani Ilala mkoa Dar es Salaam zenye thamani ya shilingi milioni 2.85 ambazo zitawasaidia wananchi hao kupata huduma za matibabu bure katika hospitali na vituo vya afya nchini.

Akizungumza leo Juni 3, 2024 mara baada ya hafla hiyo iliyofanyika kwenye Zahanati ya Vingunguti Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Ilala Alhaj Said Side alisema mtaji wa mwanadamu yeyote ni afya hivyo Taasisi ya Kumbilamoto Foundation imejali afya za wananchi wa Vingunguti ni jambo la kumshukuru  Mwenyenzi Mungu kwa kuwaza na kutekeleza jambo hili na linapaswa kuigwa na taasisi nyingine.

"kadi ya Bima ya afya ni muhimu  unaweza ukaitumia kupata matibabu mpaka ya shilingi 700,000 au milioni  kwa ajii ya vipimo peke yake hivyo wananchi wana umuhimu wa kukata bima ya afya tunaishukuru na Taasisi ya Kumbilamoto Foundation kwa kujali wananchi wa kata ya Vingunguti" alisema Sidde  


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ndugu Omary Kumbilamoto alisema Kumbilamoto Foundation imeanzishwa mwaka 2021 na kusajiliwa mwaka 2022 na inatoa huduma za kijamii sehemu zote nchini ikiwemo kuchimba visima na kusaidia makundi maalum wakiwemo Wazee Wajane na Vijana  ili kuondoa changamoto zao.

Aidha Kumbilamoto ameongeza kuwa miaka mitatu ya Dkt.Samia Suluhu Hassan nchi yetu imepata mambo makubwa ya maendeleo ambapo alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Jamary Mrisho Satura na Mbunge wa Segerea Bonnah Ladslaus Kamoli kwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo Kata ya Vingunguti na jimbo la Segerea kwa ujumla .

Nae Katibu wa Taasisi ya Kumbilamoto Foundation Alex Buberwa alisema alisema taasisi hiyo imejikita zaidi kusaidia jamii na leo hii wametoa bima za afya kwa wananchi 114 waliopo kwenye mitaa sita ya Vingunguti ikiwemo Mtakuja, Majengo Mtambani, Butiama, Miembeni na Kombo lengo kuu likiwa ni kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo waweze kuzitumia kadi hizo katika huduma ya afya.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Vingunguti ISACK MAKUNDI alisema kwa sasa Zahanati ya Vingunguti inatoa huduma masaa 24 baadhi ya huduma hizo ni Kinywa na Meno, Tiba ya mionzi (Utrasound ), Wodi ya Wazazi kwa ajili ya kuzalisha, kiliniki ya Baba Mama na Mtoto,TB na Ukoma ,Upasuaji mdogo pamoja na matibabu ya wagonjwa wa nje.


 

Post a Comment

0 Comments