Wananchi watakiwa kuheshimu na kulinda vyanzo vya Maji.Na John Walter-Manyara

Wananchi na wadau wa mikoa ya Manyara na Arusha wanaofanya shughuli zao katika bonde la ziwa Manyara wameomba bodi ya maji ya  bonde la kati kuweka mipaka halisi ya vyanzo vya maji ili kuepuka kusumbuliwa na pia kusaidia kudhibiditi uharibifu unaotokana na shughuli za binadamu. 

Wametoa wito huo katika kikao cha uundaji wa kamati ya kidaka maji cha ziwa Manyara kilichofanyika  mjini Babati ikiwa ni wiki chache tangu kutokea kwa tukio la kufurika ziwa Manyara na kuharibu mali na makazi ya watu. 

Mkulima kutoka bonde la Kiru wilaya ya Babati Jitu Vrajlal Soni ambaye ni Kaimu mwenyekiti wa baraza la kilimo taifa amesema suala la maji ni muhimu kwa Wadau wa kilimo na mifugo na kwamba changamoto iliyopo ni uharibifu wa Mazingira maeneo yanayozunguka kidaka Maji cha ziwa Manyara kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu  bila kuzingatia sheria.

"Muhimu zaidi ni kuwekwa mipaka halisi kwenye kila chanzo cha maji na iheshimiwe " alisema Jituson

Akizungumzia ombi hilo Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya maji ya bonde la kati Mhandisi Mwita Chacha, amesema changamoto kubwa inatokana na mkanganyiko wa tafsiri kuhusu mipaka ya aina ya chanzo cha maji. 

"Changamoto kubwa katika kidaka Maji cha ziwa Manyara ni shughuli za kilimo ambazo zinafanyika ndani ya mita 60 ya mito,maziwa, hivyo kamati hii iliyoundwa itachangia Sana katika kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji" alisema Chacha

Amesema bodi ya maji za Mabonde ziliundwa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ili kuweza kusimamia rasilimali za maji nchini ili ziweze kuwa endelevu.

Chacha amesema sheria hizo zipo katika ngazi kuu tano ambazo ni ngazi ya Kitaifa, ngazi ya bodi za Mabonde, kamati za vidaka Maji, kamati za vidaka maji vidogo na Jumuiya za watumia maji.

Kwa Upande wake afisa Maendeleo ya Jamii kutoka bodi ya Maji bonde la kati Nelea Bundala, amesema kupitia Viongozi mbalimbali wa vijiji, kisiasa na Wadau wengine wa maji wakiunganisha nguvu kwa pamoja kidaka maji cha  ziwa Manyara kitanusurika na kuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mgeni rasmi katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema elimu inahitajika zaidi kwa wananchi kuanzia ngazi za vitongoji, Kijij, kata, tarafa, wilaya mkoa hadi taifa juu ya sheria iliyopo ya kufanya shughuli nje ya mita 60 toka chanzo cha maji ya ili kuvinusuru  vyanzo hivyo.

Aidha Twange ameahidi ushirikiano kwa kamati hiyo mpya yenye jukumu la kuratibu mipango na mikakati ya kulinda ziwa Manyara dhidi ya uharibifu wa shughuli za binadamu. 

Kaulimbiu "Utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu letu sote".


Post a Comment

0 Comments