F Ileje wajikita kupunguza udumavu | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ileje wajikita kupunguza udumavu


Na Baraka Messa


PROGRAMU jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inasisitiza lishe toshelezi kwa watoto chini ya miaka nane kwa sababu ni usalama na uhakika wa makuzi ya mtoto kimwili na kiakili

Wilaya ya Ileje ni miongoni mwa wilaya inayoongoza kwa uzalishaji mazao mbalimbali ya chakula pamoja na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa katika mkoa wa Songwe,bado kumekuwa na changamoto ya kuongezeka kwa tataizo la Udumavu kwa watoto hususani wenye umri chini ya miaka nane.

Takwimu zinaonyesha kuwa  watoto 7018 wenye umri chini ya miaka 5 sawa na asilimia 31.9 wanaudumavu unaosababishwa na kutokula mlo kamili katika Wilaya hiyo inayosifika kwa upatikanaji maziwa yatokanayo na ng'ombe wa kisasa na kianyeji, upatikanaji mazao ya vyakula kama mahindi, viazi, mtama , mazao ya mboga mboga na uzalishaji mazao ya matunda hasa para chichi.

Baada ya kubainika kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaoishi na udumavu serikali imejipanga kutoa elimu ya kijiji kwa kijiji kuelimisha wananchi namna ya kutumia vyakula wanavyozalisha au vinavyopatikana katika maeneo yao kutengeneza mlo kamili ambao unatakiwa kulishwa watoto chini ya miaka 5.

Afisa Lishe wa Wilaya hiyo Ester Mshana akiongea na Muungwana blog anasema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuhakikisha Udumavu unapungu kwa kiasi kikubwa, kwa upande wa wilaya ya Ileje bado kuna changamoto kubwa jambo ambalo limewasukuma kuongeza zaidi nguvu ya elimu katika vijiji  vyote ndani ya wilaya hiyo.

“Hali sio nzuri kwa Wilaya yetu ya Ileje watoto 7018 chini ya miaka 5 sawa na asilimia 31.9 wanaudumavu unaosababishwa na kutokuzingatia ulaji wa mlo kamili licha ya wilaya hii kuwa na upatikanaji wa vyakula muhimu katika ukuaji wa motto”anasema Mshana.

Mshana amesema wamejipanga kutoa  elimu kwa vitendo kwa wanawake na wanaume kuhusu aina mbalimbali za vyakula rafiki kwa watoto na namna ya kuvianda ili kufanikisha lengo la kupunguza udumavu mpaka mashuleni.

“Tunatarajia elimu tukayoitoa kwa  wananchi wa Ileje kila Kijiji changamoto ya udumavu itapungua kutoka asilimia 31.9 mpaka asilimia 20 kufikia mwaka ujao wa fedha kwani” anasema tumeiweka kama ajenda ya kimkakati," ameongeza Mshana.

Anaeleza kuwa baada ya kuzifikia kata  zote 18 zilizopo katika Wilaya hiyo, hivi sasa wanahamishia nguvu ngazi ya vijiji  vyote kuweka mkazo wa elimu inayoenda sambamba na vitendo namna ya kuanda vyakula vyenye Lishe kwa watoto chini ya miaka 5.

Anazitaja kata  za Bupigu, Isongole, Luswisi na Ngulilo kuwa ndizo zimeathiriwa zaidi na changamoto kubwa ya udumavu kwa  watoto chini ya miaka 5 .

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Farida Mgomi amesema licha ya wilaya hiyo kuwa na aina mbalimbali ya vyakula kuwa bado udumavu nitishio , hivyo kuahidi kusimamia kampeni ya kutoa elimu Kijiji kwa Kijij  wakishirikiana na watalamu wa lishe .

Anasema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali kuhakikisha udumavu unapungua kwa kiasi kikubwa wamegundua kuwa kuna baadhi ya wazazi wanawanywesha watoto wadogo pombe za kienyeji jambo linalorudisha nyuma kuwasaidia watoto.

“Tumebaini jitihada za kupambana na udumavu zinakwamishwa na baadhi ya wanawake ambao badala yakuwapa vyakula rafiki watoto wanawanywesha pombe za kienyeji na kwenda nao virabuni, atakayebainika sheria itashughulika nao”anasema Mgomi.

Mkazi wa kijiji cha Kalembo wilayani humo Magidalena Mtambo anashauri sheria itungwe sheria kali itakayowabana wazazi watakaobainika kwenda na watoto virabuni na kuwanywesha pombe ikiwepo kufungwa jela miezi 6.

Naye Japheti Simbeye anasema ili kukabiliana na udumavu, wanaume pia wanatakiwa kufuatilia maendeleo ya makuzi ya watoto wao sambamba na utoaji wa fedha za matumizi kununulia vyakula ambavyo watoto wanatakiwa kula ili kuimarisha afya zao.

Akiwa katika ziara zake  Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo anawasisitiza wananchi kuzingatia lishe bora kwa watoto pamoja na kwa mama wajawazito.

“Kuna suala la lishe limekuwa changamoto  kwenye mkoa wetu. Lishe bora inawajenga watoto wetu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, lakini mtoto anajengwa zile  siku 1000 za mtoto tangu mimba itungwe”

Pia akizungumza kwenye mabaraza ya madiwa hivi karibuni Chongolo amewataka madiwani wa halmashauri zote ndani ya mkoa wa huo kuibeba ajenda ya lishe kwenye vikao vyao ,kuona namna bora ya kukabiliana au kuondoa kabisa hali hii ambayo ipo kwa sasa.

"Ni aibu kwa mkoa wetu kuutaja kuwa na changamoto ya udumavu na utapiamlo kisa ukosefu wa lishe wakati tunasifika kwa uzaishaji wa aina mbalimbali ya vyakula hii haikubaliki Kila mmoja awajibike kuondoa changamoto,"amesema Chongolo.

Aidha amewataka waganga wakuu wa wilaya kupanga ratiba ya kutoa elimu kwa wananchi wajuwe matumizi ya vyakula wanavyozalisha ili waondokane na udumavu na utapiamlo.

"Tumekuwa tukilalamika wanafunzi kufeli bila kuangalia aina ya vyakula wanavyokula ambavyo si mlo kamili na mtoto hawezi fanya vizuri embu hii ajenda iwe ya kudumu," amesema

Aidha katika maeneo yote ambayo  amezungumza na wananchi  amewasisitiza wazazi kupinga  na kuibua vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, vipigo na mimba za utotoni.

Mratibu wa mradi wa Shirika la Save the Children John Tobongo anasema wakishirikiana na Serikali baada ya Progamm Jumuishi ya Malezi , Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kuzinduliwa kitaifa 2021 wakishirikiana na Watalaam wa lishe , mipango, maendeleo ya jamii na ustawi wa Jamii ngazi ya Wilaya kuhakikisha Viongozi wa Kata na vijiji wanapata elimu kuhusu masuala ya lishe pamoja na umuhimu wa malezi bora kwa watoto kuanzia miaka 0 mpaka miaka 8.

"Lengo kubwa la kuwapa elimu ya Malezi,  Makuzi  na Maendeleo ya wali ya Mtoto Viongozi wa Kata na Vijiji ni kutokana na viongozi hawa kuwa karibu na Wananchi ambapo tunategemea elimu itawafikia Wananchi kirahisi kupitia mikutano mbalimbali na kwenye shughuli za maendeleo za kila Siku,

Lakini pia Viongozi wa vijiji huhusika kwenye michakato ya uibuaji na upangaji bajet kwenye maeneo yao hivyo tunawapatia elimu ya kuibua vipaumbele vinavyo husu malezi ya watoto kuanzia ngazi ya chini ambapo vingine vitatatuliwa ngazi za Vijiji Kata na vingine vitapelekwa ngazi ya wilaya , Mkoa mpaka Taifa"  anasema Tobongo.

"Watalaam wa Sayansi ya Makuzi ya binadamu wanatuambia kwamba mtoto anakua kiakili anapokuwa katika umri huo na napofikisha miaka 6 ukuaji wa akili kwa maana ya ubongo umbo lake na seli za muunganiko wake vinaimalika kwa asimia 90" anaeleza 



Post a Comment

0 Comments