F Paulina Gekul awaonya wanaomchafua kwenye mitandao. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Paulina Gekul awaonya wanaomchafua kwenye mitandao.



Na John Walter -Babati 

Aliyewahi kuwa naibu wa wizara ya Sheria na Katiba ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Babati Mji mkoani Manyara  Paulina Gekul amejitokeza hadharani kuwaambia wananchi kuwa hakuhusika na tuhuma zilizokuwa zikimkabili  katika kesi ya udhalilishaji wa kijana Hashimu Ally mkazi wa mjini Babati.

Gekul amekemea watu wanaoendelea kumchafua katika mitandao ya kijamii  akiwataka waache kufanya hivyo mara moja.

Amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Stendi ya Zamani wilayani Babati akielezea Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka wa fedha 2020 hadi 2024.

"Ajali inampata mtu yeyote nami  nashukuru Tume ya Haki za Binadamu kwa kutoa kauli kuwa sikuhusika" Alisema Gekul.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wananchi wanaridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya afya ambapo majengo ya hospitali ya halmashauri ya mji wa Babati (Mrara) yamekarabatiwa na mengine kujengwa upya na kuwekwa vifaa muhimu katika wodi ya wagonjwa wa dharura vilivyogharimu zaidi ya  Milioni 300.

"Hapakuwa na wodi ya dharura awali lakini kwa sasa majeruhi wa ajali mbalimbali za barabarani wanahudumiwa na kulazwa katika wodi hiyo." Alisisitiza Gekul.

Pamoja na hayo kupitia taarifa kutoka Ofisi ya Mbunge Jimbo la Babati Mjini Mbunge huyo alisema hivi karibuni ataitisha  mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tuhuma iliyokuwa inamkabili.

Post a Comment

0 Comments