F UVCCM yawaonya Viongozi wasiotimiza wajibu wao. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

UVCCM yawaonya Viongozi wasiotimiza wajibu wao.



Na John Walter -Babati 

Jumuiya ya umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Babati vijijini Mkoa wa Manyara, imewaonya baadhi viongozi wa serikali na chama kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea na badala yake wametakiwa kuwa wadilifu na waaminifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Babati vijijini Solomon Mpaki wakati akizungumza na waandishi wa Habari akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua Miradi ya Maendeleo katika kata ya Madunga.

Amesema baadhi ya viongozi wa serikali na chama wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo.

“Tunatoa maelekezo kwa viongozi wote wa Serikali na Chama, wajitahidi kwa hali na mali miradi inapokuja,fedha zinapotolewa na Serikali kuhakikisha wanatumia fedha hizo ipasavyo na ikamilike kama ilivyokusudiwa, vinginevyo hatutakuwa na salia mtume kama utakuwa hautimizi wajibu" alisema Mpaki 

Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatumia nguvu kubwa na muda mwingine hata usingizi hapati kwa ajili ya Watanzania hivyo hawatomvumilia yeyote anayekwamisha jitihada hizo.

Mpaki akiwa na wajumbe wa kamati ya utekelezaji UVCCM, wamekagua Maendeleo ya mradi wa ujenzi madarasa manne, matundu nane ya vyoo katika shule ya Sekondari Utwari yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 114, ukiwa ni Mpango wa kuihamisha shule hiyo iliyopo bondeni kwa kuwa kipindi cha mvua wanafunzi hukumbana na kadhia ya maji.

Aidha wamekagua mradi mkubwa wa maji Ziwa Madunga unaosimamiwa na wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira vijijini -RUWASA ambao unaotarajiwa kutumia Shilingi Bilioni 5 na kuhudumia kata za ukanda wa juu tarafa ya Bashnet.

Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Utwari  Emmanuel Mdee  ameishukuru serikali kwa kuwajengea madarasa hayo kwa kuwa kipindi cha mvua wengi huwa wanapitwa na masomo kwa sababu ya maji kujaa katika eneo la shule.

Naye mmoja wa wazazi Faustin Ombay amesema wanampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali kwani mradi huo ni mkombozi kwao kwa kuwa Mazingira ya shule sio rafiki.

Post a Comment

0 Comments