Wananchi wa Bagara waanza kulitumia daraja jipya.Na John Walter -Babati 

Wananchi wa kata ya Bagara mjini Babati wameondokana na adha ya mawasiliano ya barabara waliokuwa wakiipata kipindi cha mvua baada ya wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA kujenga daraja kubwa la Milioni 97.9 fedha za dharura kutoka serikali kuu.

Akiweka jiwe la msingi katika daraja hilo mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema serikali inazungumza kwa kuonyesha vitu vilivyofanyika na kwa yeyote anayesema haifanyi kazi anatakiwa akapimwe akili yake hospitali.

"Kama hili daraja mwaka jana halikuwepo,limejengwa katika miaka mitatu ya Mama Samia halafu unasema serikali haijafanya kazi hilo ni tatizo, kwa hiyo naomba nyie wananchi vitu vingine mnasikiliza tu kama ngoma zinavyopigwa, zingine zinapigwa na mlevi" alisema Twange

Amesema katika bajeti mpya ya mwaka 2024-2025 serikali imepanga kufanya mambo makubwa zaidi katika kila sekta hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na serikali yao.

Meneja wa TARURA wilaya ya Babati Mhandisi Aloyce Nombo ameeleza kuwa, Barabara hiyo ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi kwani inatumika kwa ajili ya usafiri wa Magari ya abiria, mizigo na watembea kwa miguu kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Babati.


Mwenyekiti wa mtaa wa Ngarenaro lilipojengwa boksi  kalavati hilo Samweli Ditto amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia fedha za Ujenzi.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi -CCM kata ya Bagara Benny Mshana amepongeza kazi iliyofanywa na TARURA huku akiagiza mapungufu yaliyopo yarebishwe mapema.

Daraja hilo linatarajiwa kuwekwa jiwe la uzinduzi na mbio za Mwenge wa Uhuru unaoingia mkoani Manyara kuanzia  Julai 12, 2024 ukiwa na Kaulimbiu, Tunza Mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa Ujenzi wa taifa endelevu.


Post a Comment

0 Comments