Na John Walter -Babati
Watu watatu wamenusurika kifo baada ya gari dogo walilokuwa nalo kushambuliwa na kuchomwa moto na Wananchi katika Kijiji cha Sharmo kata ya Arri Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoa wa Manyara, wakidhaniwa kuwa ni wahusika wa utekaji na kuuza figo za binadamu.
Akizungumza katika eneo la tukio, mwenyekiti wa Kijiji cha Sharmo Daudi Amsi, amesema tukio hilo limetokea Agosti 16,2024 majira ya saa 2:30 usiku baada ya wananchi kupiga yowe wakidai kuna watu wasiowaelewa kijijini hapo wakiwa kwenye gari dogo aina ya Corrola yenye namba za usajili T 360 AJH lililokuwa limesimama barabarani.
Mwenyekiti huyo amesema jitihada za askari mgambo zilisaidia kuwanusuru watu hao kutoka kwenye mikono ya umati wa wananchi hao waliokuwa na jazba.
Amsi amesema umati wa Wananchi usiku huo ulikuwa mkubwa na kwamba ilikuwa ni ngumu kuwatuliza hivyo alipiga simu Polisi ili kupata msaada japo tayari gari lilishateketezwa na moto.
Mwenyekiti huyo ameeleza vitu vilivyowapa hofu wananchi ni Shanga, vibuyu na vichupa vidogodogo walivyovikuta ndani ya gari hilo.
"Baada ya polisi kufika eneo la tukio waliwahoji watu hao wakijitambulisha ni watumishi wa Mungu na kwamba walikuwa wakirejea mjini Babati baada ya kutoka kwenye mkutano wa injili Kijiji cha Hoshani, gari lao lilizimika baada ya kuisha mafuta" alisema Mwenyekiti
Ni tukio la pili linatokea katika mkoa wa Manyara likiwa na sura inayofanana, kwani katika wilaya ya Mbulu pia gari lilichomwa moto na Wananchi na kuwashambulia watu waliodhaniwa kutaka kuwateka watoto huku jeshi la polisi mkoa wa Manyara likisema hakuna taarifa za utekaji watu.
Akitoa maoni yake, Mchungaji Josiah Sumaye amesema Kuna hofu imejengwa kwa Wananchi kupitia jumbe zinazoenabazwa kwenye simu kwamba kuna watu wanateka watu na kutoa figo zao na kuziuza.
0 Comments