Na John Walter -Babati
Mkuu wa wilaya ya Babati Emmanuela Kaganda amezindua Kampeni ya “Tuwaambie kabla hawajaharibiwa” ambayo imezinduliwa kimkoa katika Shule ya Sekondari Babati Day iliyopo Mjini Babati mkoani Manyara.
Kampeni hiyo inayosimamiwa na dawati la jinsia na watoto polisi mkoa wa Manyara imelenga kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Kaganda amelipongeza Jeshi la polisi kwa kuja na kampeni hiyo inayotekelezwa nchi nzima na kwamba ikisimamiwa kikamilifu italeta matokeo mazuri.
Aidha aliwasisitiza wanafunzi kutorubuniwa na kutofumbia macho vitendo vya ukatili ambavyo kimsingi vinakatisha ndoto za maisha yao, badala yake kutoa taarifa za viashiria vya matukio ya ukatili kwa Jeshi la Polisi, walimu au kwa watu wanaowaamini.
Kwa Upande mwingine mkuu wa wilaya aliwasihi Wanafunzi kurizika na hali walizonazo katika familia zao na kuacha kuishi maisha ya kupiga wengine kwa kuwa ndiyo mwanzo wa vishawishi.
“Jukumu lenu ninyi kama wanafunzi ni kusoma hivyo mnatakiwa kuongeza juhudi katika masomo yenu ili kutimiza ndoto za maisha yenu ya baadaye” alisema Kaganda.
Akitoa taarifa kuhusu kampeni hiyo kamishna msaidizi wa polisi, mkuu wa Jeshi la akiba mkoa wa Manyara Kija mkoi amesema maafisa polisi ngazi ya Kata katika kata 142 mkoani humo wataendelea kutoa Elimu kwenye maeneo yao.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari “Babati Day” amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kwa ushirikiano unaoendelea hususani katika utoaji wa elimu mbalimbali kwa wanafunzi katika huku akiomba iwe endelevu kwani imekuwa ikisaidia kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.
0 Comments