Na John Walter -Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati mjini Mheshimiwa Paulina Gekul amewataka Vijana waipende nchi yao kwa kuwa wazalendo na kutii mamlaka zilizopo.
Gekul ametoa Rai hiyo kwa Vijana wa kata ya Mutuka na Nangara Jimboni humo akiwa katika ziara yake ya kugawa vifaa vya michezo kwenye mitaa na vijiji kuelekea Dr. Samia & Gekul Cup yenye lengo la kuibua vipaji vipya vya soka na hatimaye kupata timu ya mpira wa miguu itakayowakilisha mji wa Babati kwenye ligi kuu Tanzania bara.
Gekul amewataka Vijana hao kujituma kwa kufanya kazi halali waweze kujimudu na familia zao na kuwaepuka baadhi ya watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Gekul amegawa mipira na jezi, vifaa ambavyo amevikabidhi kwa Vijana hao kupitia Viongozi wao ili vitunzwe na kutumiwa na wengine siku zijazo.
Uzinduzi wa michuano ya Dkt Samia & Gekul Cup 2024, itazinduliwa Rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati.
Aidha Mashindano hayo yataenda sambamba na uhamasishaji wa vijana na Wanawake kushiriki na kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa pamoja na kujiandikisha kwenye mfumo wa Kieletroniki Chama cha Mapinduzi.
Gekul amesema hakuna Chama cha siasa kinachoweza kumsaidia Kijana zaidi ya chama cha Mapinduzi na kwamba hata nchi nyingi za Afrika zimesaidiwa kupata uhuru na Chama hicho tawala.
Hata hivyo Vijana wa Chem Chem na Mutuka wamempongeza Mbunge kwa kuwakumbuka katika Soka huku wakimuahidi kutumia mashindano hayo kuonesha vipaji vyao.
Wasimamizi wa mashindano hayo Chama cha Soka wilaya ya Babati kupitia kwa mwenyekiti Gerald Mtui wamesema watahakikisha wanasimamia kanuni na Sheria zote za Soka ili lengo la Mbunge kupata vipaji vipya vya soka litimie.
Mtui amesema pia katika michuano hiyo watachukua Vijana wadogo wenye umri chini ya miaka 15 na wale wenye umri chini ya miaka 20.
0 Comments