F DC Mpogolo awataka wajasiriamali kutumia vizuri mikopo ya halmashari kukuza biashara zao | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

DC Mpogolo awataka wajasiriamali kutumia vizuri mikopo ya halmashari kukuza biashara zao


Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka wajasiriamali kutumia vizuri mikopo wanayokopa  katika halmashari ya jiji  kukuza biashara zao.

Mpogolo ametoa wito huo wakati anafunga mafunzo ya siku tatu kwa wajasiriamali 600  yaliyodhaminiwa na kufundishwa na wakufunzi katika chuo cha Biashara CBE  wilayani  Ilala Mkoani Dar es salaam.

Amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan amerudisha fursa ya mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu na wilaya ya Ilala ina zaidi ya bilioni 11 ili kuyawezesha makundi hayo.

Mikopo ambayo kwa sasa itatolewa kwa makundi matatu katika ukopaji kwa viwango tofauti kwa waombaji kuanzia kiasi cha shilingi  laki 5 hadi milioni 10 kwa kundi la kwanza, kundi la pili milioni 10 hadi milioni 50 na kundi la tatu milioni 50 hadi 150.

Ameeleza kuwa kupitia Mikopo hiyo kundi kubwa la wanawake watanufaika kwa kuwa wana muamko wa vikundi tofauti na kundi la wanaume ambao ni wachache waliojikita katika vikundi vya uwekaji fedha.

Akizungumzia juu ya mafunzo hayo yanayotolewa na chuo cha biashara Mpogolo amewahimiza wanufaika wayatumie vizuri ili kuleta tija katika biashara zao kwa kuwa wabunifu zaidi.

Amesema kupitia mafunzo waliyopata kwa siku tatu juu ya elimu ya masoko waweze kutafuta masoko mapya hasa kwa wafanyakazi maofisi ili kuwafikishia mahitaji  kwa urahisi.

 Kuhusu ubunifu wa vifurushi amewahimiza kutumia njia rafiki ya kufunga bidhaa zao kulingana na uhitaji wa mteja na bei ya soko ili wateja waweze kumudu kununua tofauti ya soko la sasa kuangalia mteja mmoja.

Aidha Mpogolo amezungumzia suala la matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wajasiriamali kutangaza biashara zao kisasa ili kuwafikia wateja wengi kwa urahisi.

Mpogolo ameongeza kuwa  halmashauri ya jiji la Ilala ina zaidi ya asilimia 90 ni wafanyabiashara katika masoko mbalimbali na wateja wake wanatoka katika nchi jirani, mikoani na wilaya nyingine za mkoa wa Dar es salaam.

Hali inayongeza ukuaji wa biashara na ushindani katika masoko kwa wajasiriamali kuhitaji mitaji ya uwakika.

Aidha katika Mafunzo hayo Mpogolo amewasihi wajasiriamali hao kutumia mikopo vizuri  kujiletea maendeleo wasiitumie kwa mambo ya anasa.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ameonya kukimbilia mikopo ya kausha damu  ambayo imekua na athari kwa jamii  kutoka na masharti ya urejeshaji na kusababisha migogoro katika familia nyingi hali inayosababisha umasiki zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Biashara CBE Prof Edda Lwoga amesema wameamua kudhamini na kufundisha mafunzo hayo ya siku tatu ili kuongeza uelewa kwa wajasiriamali kufanya biashara zao kisasa na kukuza uchumi.

Jambo ambalo Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amempongeza Mkuu wa Chuo cha CBE Prof Edda Lwoga, halmashauri ya jiji la ilala na Equity Bank na kuvitaka vyuo na taasisi za fedha nyingine kuiga mfano huo ili kurudisha kwa jamii ya watanzania.



 

Post a Comment

0 Comments