Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe Zacharia Mwansasu amewataka walimu kuanza maandalizi ya kustaafu mapema wakati bado wakiwa na nguvu ili kuepukana na tatizo la msongo wa mawazo baada ya kustaafu linalopekelea maradhi kutokana na kushindwa kufanya maandalizi ya kustaafu wakati bado wakiwa na nguvu ya kufanya kazini.
DC Mwansasu ametoa wito huo wakati akizungumza na walimu takribani 1208 waliokusanyika kwenye ofisi za halmashauri hiyo katika siku ya mwalimu duniani kwa lengo la kupongezana na kukumbushana maswala mbalimbali ikiwemo malengo ya serikali pamoja na halmashauri katika kuendelea kukuza viwango vya taaluma kwa wanafunzi wilayani humo.
"Ndugu walimu nawakumbusha kuanza maandalizi ya kustaafu mkiwa bado mna nguvu kwasababu walimu wengi wamekuwa wakipata msongo wa mawazo mara tu baada ya kustaafu kutokana na kushindwa kufanya maandalizi kustaafu mapema"amesema DC Mwansasu
Mwansasu amewakumbusha walimu katika maswala ya mikopo ambapo ametoa wito kuepuka mikopo isiyokuwa na malengo na kuwataka kuhakikisha wanajiridhisha na kuielewa mikataba ya mikopo wanayohitaji kuingia ili kuepukana na mikopo umiza.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe Peter Nyanja amesema ataendelea kuhakikisha walimu wanapata stahiki zao zote ndani ya halmashauri hiyo huku akiwataka walimu kuendelea kuongeza ufanisi kwenye kazi na kuhakikisha taaluma inaendelea kuwa nzuri kwa kufuta daraja la sifuri na daraja la nne kwa elimu ya sekondari huku kwa elimu ya msingi ufaulu ukiwa zaidi ya 95%
Dkt.Festo Dugange ni Mbunge wa jimbo la Wanging'ombe amesema serikali itaendelea kuwaheshimu walimu kutokana na majukumu makubwa wanayoyafanya kwenye jamii ambapo wakati mwingine wamekuwa wakifanya majukumu mengi nje ya ualimu kwenye maeneo yao kutokana na uhaba wa watumishi kwenye vijiji.
"Kuna maeneo mengine unaweza ukakutana na mwalimu yeye ni mwalimu wa shule lakini ni kaimu mtenadaji wa kijiji lakini ni kaimu afisa misitu ni kaimu afisa mifugo,ninachotaka kusema nikatika wataalamu wa serikali ninyi walimu ndio mmekuwa na maeneo mengi mnafanya kazi kuliko wataalamu wengine"amesema Dugange
Kwa upande wao walimu wamemshukuru mkurugenzi kwa kuendelea kujenga umoja ndani ya halmashauri ambapo wameahidi kuongeza viwango vya ufaulu kwa wanafunzi ili kufikia malengo waliojiwekea.
Aidha Katika salamu za wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa walimu waziri wa elimu Prof.Adolf Mkenda akizungumza na vyombo vya habari mkoani Njombe, pamoja na kuwashukuru walimu na kuwatia moyo kwa kazi wanayoifanya lakini pia amewata kuepuka visa vya baadhi ya walimu wanaokengeuka na kusahau kazi kubwa wanayaoifanya kwa kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
"Walimu wameendelea kujituma na kufanya kazi kwa bidii,weledi na uadilifu mkubwa visa vichache vinavyotajwa mara chache vya baadhi ya walimu wanaokengeuka visitumike kwa namna yeyote kuwakusanya walimu wote na kusahau kazi kubwa sana wanayoifanya,serikali inaendelea na juhudi mbali mbali za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia"amesema Prof.Mkenda



