Na John Walter -Babati
Wakati zoezi la kupiga kura likiendelea maeneo mbalimbali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Babati Mjini kimedai mawakala wake wapatao 63 wameondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.
Akizungumza na Waandishi wa habari mwenyekiti wa Chama Cha Dermokrasia na Mandeleo {Chadema} Jimbo la Babati mjini Valentina Shayo amesema kuwa mawakala wao wote wameondolewa kwa maagizo ya afisa uchaguzi aliyepokea maelekezo kutoka TAMISEMI.
Mwanasheria wa CHADEMA kanda ya kaskazini Thadey Lister amesema pia wagombea wao wamekatazwa kuingia kwenye vituo kufuatilia zoezi la upigaji kura na kwamba wanaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu.
Kwa Upande wake msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Babati mjini Shabani Mpendu amesema walioondolewa kwenye vituo ni mawakala ambao pia ni wagombea na sio wote kama CHADEMA walivyodai.
"Wagombea walioondoleaa hawazidi 10" alisisitiza Mpendu
Amesema hayo sio maamuzi ya TAMISEMI wala mkoa bali ni kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024.
Hata hivyo baadhi ya Mawakala wa CHADEMA na CCM waliozungumza na kituo hiki wakiwa kwenye vituo vyao wamesema kila kitu kipo sawa na hakuna changamoto yoyote mpaka sasa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo chake cha Mrara, amewahakikishia Wananchi kuwa zoezi la uchaguzi litaenda salama hivyo wananchi waendelee na shughuli zao wakati wanasubiri matokeo.
0 Comments