F Gekul: Rais Dkt. Samia Hana Deni Babati, Miradi Yatekelezwa kwa Ufanisi. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Gekul: Rais Dkt. Samia Hana Deni Babati, Miradi Yatekelezwa kwa Ufanisi.


Na John Walter -Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mheshimiwa Paulina Gekul, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hana deni kwa wananchi wa Babati, kwani miradi yote ya maendeleo imefanikiwa kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Akiwa kwenye ziara katika Kata ya Bonga, Gekul amewashukuru wananchi kwa kuiamini serikali na kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato. 

Pia alipata nafasi ya kuzungumza na mabalozi wa maeneo hayo, akiwapongeza kwa mchango wao katika maendeleo ya jamii.

Gekul amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza kikamilifu katika sekta muhimu kama afya, elimu, na kilimo.

Ameeleza kuwa serikali imejenga zahanati na vituo vya afya, kuboresha huduma za elimu, na kusaidia wakulima kwa kutoa mbegu za ruzuku. 

Aidha, amesema kuwa barabara zimeboreshwa, maji safi yamefikishwa kwa wananchi, na umeme umesambazwa katika vijiji na mitaa yote ya Jimbo la Babati Mjini, huku wakisubiri umeme jazilizi kwa ajili ya vitongoji.

Kwa mujibu wa Gekul, deni lililopo kwa wananchi ni kuhakikisha wanamlipa Rais Dkt. Samia kwa kumpigia kura zote ifikapo Oktoba 2025, ili aendelee kuongoza nchi na kuwaletea maendeleo zaidi.

Akiwa katika Tawi la Logia, Kata ya Sigino, aliwapongeza mabalozi kwa kutambuliwa rasmi kama wapiga kura na kuwahimiza kuwapitisha wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge kwenye maeneo yao bila rushwa pindi muda utakapofika.

Pia aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa fedha kwa kila kata na kijiji ili kuendeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.

Gekul amewataka wananchi waendelee kuwa na imani na serikali ya Rais Dkt. Samia na kuhakikisha wanampa kura za ndio katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ili aweze kuendelea kuwatumikia kwa ufanisi.

Post a Comment

0 Comments