Na John Walter -Babati
Wananchi wa Himiti na maeneo mengine ya Kata ya Bonga, wilayani Babati, wamepata ahueni baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuahidi kufika katika maeneo hayo mnamo Februari 28 ili kushughulikia tatizo la tumbili wanaoshambulia mazao yao.
Katika mazungumzo ya simu na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Paulina Gekul, wataalamu wa TAWA wamesema wamepokea malalamiko ya wakulima na wanachukua hatua za haraka kutathmini hali halisi.
Wananchi, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, wamemueleza Mbunge wao jinsi tumbili hao wanavyoharibu mazao yao, hususan mahindi na ndizi.
Baadhi yao wamesema wamekata tamaa na kuacha kulima kabisa kutokana na hasara wanayopata.
TAWA imetoa pole kwa wananchi walioathirika na kuahidi ushirikiano wa karibu ili kupata suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo.
Matarajio ya Wananchi ni kwamba kupitia timu ya wataalamu, itafanyika tathmini ya kina na kupanga mbinu bora za kukabiliana na wanyama hao waharibifu.
0 Comments