F Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre wa Padre Ephrem Malley | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre wa Padre Ephrem Malley



Na John Walter -Babati 

Leo April 24,2025 katika Kanisa la Parokia ya Utatu Mtakatifu - Maisaka, imefanyika ibada takatifu ya maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya upadre wa Padre Ephrem Joseph Malley. 

Ibada hiyo imehudhuriwa na mapadre kutoka Jimbo Katoliki la Mbulu pamoja na waumini wengi waliofika kumpa hongera Padre Ephrem kwa utumishi wake wa muda mrefu kwa Kanisa.

Katika hotuba yake, Padre Ephrem amemshukuru Mungu kwa neema ya kumwita katika daraja la upadre na kwa kumwezesha kutumikia kwa miaka yote 25 kwa uaminifu na upendo. 

Ameelezea safari yake ya utumishi tangu mwaka 2004 alipokuwa Wakili Paroko wa Parokia ya Gairo, hadi 2005. 

Kuanzia mwaka 2006 hadi 2013 alihudumu kama Baba wa Kiroho katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino- Mwanza. 

Mwaka 2013 hadi 2014 aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Masuala ya Fedha na Utawala katika Chuo Kikuu cha Bugando - Mwanza.

Kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, Padre Ephrem alikuwa Mkuu wa Shirika la Nyumba la Tanzania, Paroko wa Parokia ya Bassotu, na pia Paroko wa Parokia Ndogo ya Basodesh. 

Tangu mwaka 2021 hadi sasa, anahudumu kama Paroko wa Parokia ya Utatu Mtakatifu - Maisaka na pia ni Dekano wa Mbugwe.

Padre Ephrem, mwenye umri wa miaka 59, alizaliwa katika Kijiji cha Dirim, Wilaya ya Mbulu.

Katika ibada hiyo ya maadhimisho, alikabidhiwa zawadi mbalimbali kama ishara ya pongezi na shukrani kwa utumishi wake uliotukuka.

Tukio hili limeacha kumbukumbu ya kipekee kwa waumini wa Parokia ya Maisaka na ni ushuhuda wa uaminifu na sadaka ya maisha ya upadre kwa huduma ya Mungu na watu wake.

Post a Comment

0 Comments