F Jumuiya ya makanisa ya CCT Babati yamujumuika ibada ya ijumaa kuu. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Jumuiya ya makanisa ya CCT Babati yamujumuika ibada ya ijumaa kuu.



Na John Walter -Babati 

Jumuiya ya makanisa ya CCT imejumuika leo katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Babati Mjini, Jimbo la Babati, Dayosisi ya Kaskazini Kati. 

Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa Jimbo hilo, Mchungaji Robert Mallya, na kuhudhuriwa na waumini kutoka madhehebu mbalimbali wanachama wa CCT katika Wilaya ya Babati.

Katika ibada hiyo, maandiko kutoka Luka Mtakatifu 23:44-49 yalitumika kama msingi wa tafakari, yakielezea kifo cha Yesu Kristo na maana yake kwa wokovu wa wanadamu. 

Mchungaji Mallya alieleza kuwa, "Kifo ni njia ya kwenda mbinguni, lakini mimi kama mchungaji wenu nawashauri msiwe na haraka ya kwenda mbinguni. Tungependa kuendelea kuona vipaji vyenu, na muendelee kumtumikia Mungu duniani."

Mchungaji huyo amesisitiza kuwa leo si siku ya kuomboleza bali ya kutafakari maana ya kifo cha Yesu Kristo. 

Ameeleza kuwa tukio hilo linaonyesha upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu, ambapo Mungu alibadilisha utaratibu wa kawaida wa haki—badala ya mkosaji kuadhibiwa, Yesu alijitoa kafara ili wengine wapate uzima.

“Ijumaa Kuu ni kumbukumbu ya sadaka ya upendo wa kweli, kifo cha Yesu si mwisho bali mwanzo wa tumaini jipya kwa wanadamu,” alisema Mchungaji Mallya.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na waumini kwa wingi, ikionyesha mshikamano na moyo wa ibada miongoni mwa washiriki wa CCT katika Wilaya ya Babati.

Maombi maalum pia yalifanyika kwa ajili ya taifa, viongozi wake, na uchaguzi mkuu ujao, yakisisitiza amani, haki na umoja.

Picha mbalimbali kwenye ibada hiyo.

















Post a Comment

0 Comments