Kamati ya Fedha ya Halmashauri ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Joseph Mandoo Diwani wa Kata ya Dinamu imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Aprili 2025, ilihusisha jumla ya miradi kumi na mbili (12) yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.036,838,595.16, inayotekelezwa katika sekta za Elimu, Afya na Utawala.
Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mandoo alionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi hiyo.
“Niwaombe wataalam tuendelee kusimamia miradi hii kwa ufasaha ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mhe. Mandoo huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa karibu kati ya viongozi na wataalam ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Mhe. Mandoo pia alieleza kuwa, tangu awe Mwenyekiti wa Halmashauri kwa zaidi ya miaka kumi, hajawahi kushuhudia kiwango kikubwa cha fedha na miradi mikubwa ya kimkakati kama inavyoshuhudiwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Alisema ni wazi kuwa serikali hii imedhamiria kwa dhati kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa Serikali, Katibu Tawala wa Wilaya, Ndugu Paulo Bura, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Abubakar Kuuli, kwa usimamizi bora wa miradi hiyo.
Alimtaka kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaongezeka zaidi ili miradi yote iwe imekamilika kabla ya tarehe 30 Juni 2025.
“Tunahitaji kuhakikisha hatulali – kuanzia asubuhi hadi jioni – hadi pale miradi hii itakapokamilika kwa wakati,” alisisitiza Bura.
Ukaguzi huu umeonesha dhamira ya dhati ya Halmashauri katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia utekelezaji wa miradi yenye tija, huku viongozi wakihimiza uwajibikaji na usimamizi wa karibu katika kila hatua ya utekelezaji.
0 Comments