Na John Walter -Babati
Kijana Jamal Yusuf (28) aliyemuua mama yake mzazi, Zauda Shabani (57), amezikwa kimya kimya katika mazingira ya utata, siku chache baada ya kutekeleza mauaji hayo ya kusikitisha nyumbani kwao katika kitongoji cha Mji Mpya, kijiji cha Orngadida, kata ya Qash, wilayani Babati.
Jamal alimuua mama yake kwa kumchinja kwa kisu mnamo Aprili 12, mwaka huu saa nne asubuhi kisha naye kuuawa na Wananchi wenye hasira kali.
Taarifa kutoka kwa majirani na ndugu wa karibu zinasema kuwa marehemu hakuwa mtu wa kushirikiana na wengine, hakuwa na marafiki, hakuwa na watoto, na pia hakuwa karibu na wanawake.
Inadaiwa pia kuwa enzi za uhai wake, alikataa dini na kuacha maelekezo kwamba asizikwe kidini.
Kwa mujibu wa mashuhuda, Jamal alifukiwa kaburini kimya kimya, bila ibada yoyote, huku akiacha simanzi kubwa kwa familia na jamii inayozunguka.
Mama yake, Zauda, alizikwa kwa mujibu wa imani ya Kiislamu, huku vilio na majonzi vikishuhudiwa wakati wa mazishi.
Diwani wa kata ya Qash, Mheshimiwa Idd Gitianga, amelaani vikali tukio hilo, akiwataka viongozi wa vitongoji kuwahamasisha wananchi kukabiliana na uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, hasa kwa vijana.
Aidha, Katibu wa Kamati ya Amani dini mbalimbali wilaya ya Babati Issa Maguo, amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana, akibainisha kuwa wengi wamepotea njia kwa kuacha kwenda kwenye nyumba za ibada, kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, na malezi duni.
Wakati huo huo, kina mama katika jamii hiyo wameiomba jamii ya kidini nchini kuendelea kuliombea taifa, ili matukio ya namna hii yasijirudie.
0 Comments