F Wananchi Igagala waimarika kiuchumi,wamiliki nyumba na magari,wawili pekee wabaki TASAF | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wananchi Igagala waimarika kiuchumi,wamiliki nyumba na magari,wawili pekee wabaki TASAF

 


Wananchi wa kijiji cha Igagala halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe wameomba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwasaidia ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti (Mochwari) kwa kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kukamilisha mradi wao wenye thamani ya Milioni 501 kwa uaminifu bila kutokea vitendo vya wizi.

Ombi hilo limetolewa na wananchi wa kijiji hicho kwa Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Taifa ya TASAF Peter Ilomo mara baada ya kukagua baadhi ya majengo ya kituo cha afya Igagala ikiwemo kichomea taka,jengo la upasuaji,jengo la mama na mtoto,jengo la Maabara pamoja na nyumba mbili za watumishi kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu.

Awali mtendaji wa kata ya Ulembwe Sharifa Kunga akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji hicho amesema utekelezaji wa mpango ulianza mwaka 2015 ambapo jumla ya kaya 78 ziliandikishwa na mpaka sasa kaya mbili pekee zimebaki zikinufaika na mpango huo.


"Kupungua kwa walengwa kumetokana na sababu mbalimbali kama kuhama na kuimarika kiuchumi"amesema Sharifa Kunga

Kwa Upande wake mwenyekiti wa halmashauri  ya wilaya ya Wanging'ombe Agnetha Mpangile amesema kujengwa kwa majengo hayo kumezidi kuimarisha huduma za afya huku akishukuru TASAF kwa kubadilisha kaya maskini na kuwataka wananchi kutumia kituo hicho kikamilifu ikiwemo kuongeza idadi ya watu.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe Dkt.Peter Nyanja amesema kijiji hicho kwa sasa ni miongoni mwa vijiji vilivyoimarika kiuchumi hali iliyopelekea wanufaika wa TASAF kubaki wawili pekee.

"Ukiangalia kulia na kushoto, makazi yamebadilika sana na nyumba zao ni kisasa  na hamna tena yale mabati yale ya zamani ndio maana uchumi umeongezeka na wamebakia watu wawili TASAF nao wako mwishoni kuhitimu"amesema Dkt.Peter Nyanja


Nyanja amesema lengo lao ni kufanya kituo hicho kuwa hospitali ndogo ndio maana kwa kushirikiana na wananchi wanahitaji ongezeko la  majengo ya kutolea huduma.

"Kituo hiki kipo kwenye barabara kuu ya kwenda Makete mapaka Mbeya kwa hiyo lengo letu tunataka tukifanye kuwa hospitali ndogo ndio maana tunaomba wodi ya Wanaume,Wanawake na Mochwari na hiyo ndio dira yetu ya wilaya"amesema Nyanja


Naye Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Taifa ya TASAF Peter Ilomo amesema kupatika kwa huduma nyingi kwenye kituo hicho utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi na kupongeza kazi kubwa ya ujenzi iliyofanyika huku akiagiza utunzaji wa mali za kituo cha afya ambapo pia amesema kwa kushirikiana na serikali wanakwenda kutafuta njia bora ya kutekeleza maombi hayo.


Post a Comment

0 Comments